Wakenya wenzangu, tuwaunge mkono wasanii wetu

Hapa Kenya tumebarikiwa na wasanii wenye vipaji mbalimbali ambao tunafaa tujivunie uwepo wao katika maisha yetu. Tunao wasanii wa ucheshi, wanamziki na wengineo wanaotambulika sio hapa nchini pekee, bali pia kwenye mataifa mbali mbali ulimwenguni.

Tunao wanamuziki wanaoimba aina za kipekee za nyimbo kama vile Kapuka na Genge ambao kwa kawaida huimba kwa lugha ya mtaani maarufu Sheng. Wasanii wanaoimba kwa lugha za jamii mbali mbali za humu nchini kama vile Kijaluo, Kikuyu, Kikamba na Kiluhya pia wapo.

La kushangaza ni kwamba sisi Wakenya hatujaweza kuwaunga mkono ipasavyo wasanii wetu. Sijawahi kuelewa ni kwa nini Mkenya atalipa Shilingi elfu kumi kama kiingilio kwenye tamasha ya msanii kama vile Chris Brown ama Konshens lakini vigumu kulipa shilingi elfu moja kuingia kwenye tamasha ya msanii wa hapa kwetu. Wengi wetu wameonekana kuvutiwa zaidi na nyimbo za wasanii kutoka nchi ya Tanzania, Nigeria na mataifa ya Magharibi.

Kulingana na takwimu za hivi punde kutoka mtandao wa video na muziki wa YouTube, idadi kubwa ya Wakenya walitazama video za muziki za Bongo Flava ikilinganishwa na idadi iliyotazama video za wanamuziki kutoka Kenya. Video za mwanamziki Diamond Platinumz ndizo zilizotizamwa zilizooonekana kuwa maarufu zaidi. Kutoka Kenya, vijana wetu wa Sauti Sol ndio walioongoza kwa idadi ya video zilizotazamwa zaidi haswa video ya Unconditionally Bae ambayo wamemshirikisha Ali Kiba.

Takwimu hizi ni ishara tosha ya kwamba hatujawaenzi wasanii wetu jinsi tunavyowaenzi wasanii kutoka nchi zingine. Huenda uzalendo wetu ni wa kiwango cha chini. Kumbukeni msemo kwamba mcheza kwao hutuzwa. Wasanii wetu wamejaribu angalau kutumbuiza hapa kwetu na sioni kwa nini ni vigumu kwetu kuwatuza. Iwapo tungetaka wavume zaidi katika rubaa za kimataifa basi lazima tuonyeshe ulimwengu kuwa tunawapenda na tunawaenzi wasanii wetu.

Tukiwaenzi hapa nyumbani basi bila shaka wataenziwa ulimwenguni kote.