Mihadarati: Mimi ni mweupe kama pamba

Mwakilishi wodi ya Bofu Ahmed Salama.

Nyundo ya waziri wa usalama Fred Matiang’i ilipo gonga kufuatia agizo lake kutangaza vita dhidi ya madawa ya kulevya, operesheni ya polisi mara moja ikaanza.

Aidha kamata kamata pamoja na misako ya makaazi ya washukiwa ikatanda mjini Mombasa ambapo zaidi ya watu 15 wakaarifiwa kutiwa mikononi kwa shutuma za kuendeleza biashara ya mihadarati.

Kati ya watu tajika ambao wamepigwa kurunzi na operesheni hiyo mpaka sasa ni mwanabiashara wakubobea Ali Punjani, ambaye nyumba yake huko Nyali ilivamiwa na kusakwa na polisi pamoja na mwakilishi wodi ya Bofu, eneo bunge la Likoni Ahmed Salama.

Mjumbe huyo wa bunge la kaunti ya Mombasa alidaiwa kuhusika na biashara hiyo haramu na hatimaye maafisa wa uchunguzi walitembeza msako nyumbani kwake na mwishowe kufikishwa mahakamani kesho yake.

Hata hivyo, mahakama ya Mombasa ilimuachilia huru Ahmed Salama kwa ukosefu wa ushahidi wowote dhidi yake kumuunganisha na madai ya ulanguzi wa madawa ya kulevya.

Katika mahojiano na Pambazuko siku ya Ijumaa wiki iliyopita, mwanasiasa huyo alidai kudhulimiwa kwa kulimbikiziwa shutuma ilihali yeye hajawahi kuhusika katika biashara ya mihadarati.

“Nilipofika kituo cha polisi baada ya kuitwa na OCS na kufahamishwa kwamba kulikuwa na tuhuma za mihadarati dhidi yangu na kwamba wanataka kufanya uchunguzi, nilikubali kushirikiana nao kwa sababu mimi najijua niko mweupe kama pamba,” alisimulia.

“Na nilifuata amri zao zote walizotaka,” asema Ahmed Salama, akieleza jinsi maafisa walielekea nyumbani kwake pamoja na nyumbani kwao aliko zaliwa na kutembeza msako barabara.

“Polisi walisaka kila mahali mpaka majikoni, darini kila mahali hakuna walipoacha,” asema. Kulingana na kiongozi huyo, walipomaliza msako wao polisi walikiri kwamba hawakupata kitu chochote kinacho muunganisha na tuhuma dhidi yake lakini hata hivyo akaarifiwa kuwa alihitajika kupelekwa makao makuu ya polisi pwani kwa mahojiano na mkubwa wa polisi Mombasa Johnstone Ipara.

Anaeleza kuzungushwa kwani walipofika makao makuu ya polisi hakukuwa na mtu yeyote ikabidi apelekwe kituo cha Central, na hatimaye akaishia kutolewa hapo na kupelekwa hadi kituo cha polisi kilichoko bandari ya Mombasa ambako alizuiwa hadi siku ya pili alipopelekwa mahakamani.

Hata hivyo mwanasiasa huyu sasa anadokeza kwamba masaibu yalompata yanatokana na uhasimu unao tokota katika ulingo wa siasa za Likoni na anaelekeza kidole cha lawama kwa ‘wanasiasa’ walio msingizia kwa polisi wakiwa na nia ya kumkata maguu asishiriki msimu wa 2022.

“Mimi najua kuna mkono wa kisiasa kwa sababu 2022 inakuja na wengine wananipiga vita kwa sababu ya 2022. Hawa watu wanafikiri wao ndio wenye nguvu za kumiliki Likoni,” anadai mwanasiasa huyu maarufu pia kama ‘Bulldozer’.

Kiongozi huyu ambaye alichaguliwa mara ya kwanza kama kansela wa wodi ya Bofu mnamo 2007, kuangushwa mwaka wa 2013 na kurudishwa tena uongozini 2017 anadai kwamba mahasimu wake wa kisiasa huenda wakawa na mipango tele ya kumchafua zaidi hadhi yake.

“Najua bado hizi shughuli zinaendelea na wana mipango ya kuniwekea mabunduki na zana zozote ili nisifike 2022,” asema.

“Nimekuwa kwenye siasa miaka hii yote mbona hizi fitina zilikuwa haziji. Lakini saa hii kuna maneno ya 2022 ndio yanaleta hizi shida.”

Akosoa operesheni inayo endelezwa Kama alivyo achiliwa na mahakama Ahmed Salama ndivyo walivyo achiliwa washukiwa wengine walio kamatwa na polisi nyumbani mwa tajiri Ali Punjani.

Polisi walidai huenda watu hao akiwemo mkewe Punjani, mtoto wa ndugu yake na jamaa mwengine raia wa India wangesaidia kuangazia masuala fulani juu ya shutuma za biashara ya mihadarati.

Lakini mahakama ikatupilia mbali ombi la polisi kutaka kuwazuia zaidi ikisema kwamba hakukuwa na ushahidi wowote wa maana. Kulingana na mwakilishi Ahmed Salama, operesheni hii iliyo sifiwa kuwa itawanasa akina nyangumi wa ulanguzi wa mihadarati sasa huenda ikaishia patupu kwani maafisa wa usalama hawakamati washukiwa wapasao.

“Polisi sio kwamba hawajui wauzaji ni akina nani. Hapa likoni kuna majina yametajwa kwa muda mrefu lakini nani ameshikwa. Polisi wana wakinga hawa wauzaji na hata kushikwa kwangu ilikuwa ninafanyiwa biashara kwa kusingiziwa ili kuwaziba wauzaji madawa,” anadai.

“Hiyo operesheni inayo endelea mimi siipingi. Ni kazi nzuri sababu itasaidia jamii, lakini je watashika watu wa kweli ama watasingizia watu wengine ili wakubwa wakiondoka waendelee na biashara zao.”

“Serikali lazima mjue kwamba kuna watu wanataka kumaliza wenzao na kwa hivyo kabla hamjachukua hatua yoyote dhidi ya shutuma kwa mtu, fanyeni kazi yenu ya kipolisi kitaalamu na sio kutumiwa tu,” alimalizia.