Mkoko ndio mwanzo licha ya Bandari kutoka sare na Mathare

[Picha: Standard]

Kutoka sare 0-0 nyumbani dhidi ya washindani wao wakuu Mathare United mwishoni mwa wiki kumeharibu mfululizo wa matokeo mema ya Bandari ilotazamiwa kushinda na kudhibiti nafasi ya kwanza kikamilifu katika jedwali la ligi kuu nchini KPL.     

Mkoko ndio mwanzo umealika mauwa kwani songmbwingo ya ligi imechacha na kuzidi kuchacha.Kila timu inajituma pakubwa kuandikisha matokeo mema.

Tofauti ya alama kwa kila timu ni finyu mno na anayeteleza basi atakula huu na hasara juu.Hakuna timu rahisi kwani hata hizo goi goi zinajitahidi kwa udi na uvumba na hata kuwashangaza wapinzani wakuu walodhani ni mboga.

Msimu huu Bandari ilianza vizuri na hata sasa kuongoza lakini inaonyesha kulegeza kamba.Ilikuwa fursa mwanana kwa Bandari kuwachapa Mathare walipowakaribisha nyumbani lakini wakalazimishwa sare hivyo kupoteza alama mbili nyeti

Wasimamizi wa Bandari sharti waje na mbinu mpya ili wakarabati na waboreshe palipoharibika.Ni jambo la kuridhisha kwa timu kuweza kupata ushindi wakiwa ugenini.

Mashabiki walifurahi wakati Bandari ilipowafuga wapinzani wao wengine wakuu Kariobangi Sharks kule Nairobi na kuongoza jedwali.

Ushindi huo mwembamba wa 1-0 dhidi ya Sharks ulikuwa mtamu kama hamamu za amu kwani waliweza kulipiza kisasi cha kule Dar-es-Salaam  waliposhindwa fainali ya SportsPesa.

Bandari lazima iongoze motisha kwani watetezi Gor Mahia walio nafasi ya pili wanawafata unyo unyo.Tukumbuke Gor wako katika kinyang’anyiro cha kombe la shirikisho Afrika na wanaandiksha matokeo mema huku wakiongoza kundi lao.

Kwa mtazamo huu Gor sasa imenowa makali na itawasukuma Bandari sana.Ingawa Bandari iliwanyowa Gor walipowakaribisha Mombasa lakini kuna ngoma ya marudiano nao kule Nairobi.

Gor bila shaka itataka kulipiza kisasi na kutwaa alama zote tatu toka kwa Bandari.Hatahivyo Badari wana uwezo wa kunyakuwa alama hizo nyeti japo si rahisi.itatakikana bidii na nidhamu ya hali ya juu kuleta ufanisi.

Ni mambo yapi ambayo yataifanya Bandari kumtwaa mwanamwali wa KPL na kutawazwa bingwa wa Kenya nzima?

Kwanza,Bandari wana mdhamini thabiti tukimaanisha halmashauri ya Bandari Kenya kwa mkato KPA.Ama kweli pesa zilivunja mlima sembuse hili la kutwaa taji kwa kigezo hicho?

Sambamba na udhamini Bandari ina Mkuu wao mkurugenzi mkuu Bwana Hezron Manduku ambaye amejitowa muhanga kuhamasisha na kuwasaidia wachezaji na safu ya ufundi kwa hali na mali.

Manduku ameonyesha haya kwa vitendo kwa kutembelea timu katika kambi ya mazoezi kila mara mbali na kuhudhuria mechi zao.

Wakati Bandari ilipoingia fainali ya SportPesa kule Dar baada ya kwashangaza  Simba Sports mabingwa wa Bongo Manduku aliwatuza shilingi nusu milioni (Ksh.500.000)!

Majuzi katika hafla alowaandilia wachezaji na maafisa katika hoteli moja ya kifahari kisiwani Manduku aliwahimiza wafanye bidii katika michuano ya ligi ilobaki ili wanyakuwa taji  la KPL.Aliwapa changamoto kwa ahadi bab kubwa alotowa:-

‘Mukishinda ligi mutapanda ndege niwatembeza Ulaya kama mashujaa na watalii na kustarehe!’ aliahidi Manduku huku wachezaji na maafisa wao wakipia makofi ya kilo.

Mbali na uhakika wa udhamini kigezo mufti kilicho uti wa mgongo kwa timu yoyote Bandari pia ina sifa ya kuwa na wachezaji hodari katika sehemu zote za uchezaji toka kipa,mabeki,viungo vya kati na washambuizi.

Bandari iliwasajajili wachezaji bora sambamba na wa kimataifa walio na sifa za hali ya juu.Baadhi ya wachezaji wa kimataifa katika kikosi ni Wadri Wiliam wa Uganda, Mulumba Felly (DRC Congo) na Yema Mwana wa Afrika magharibi.

Wachezaji wengine hodari ni  Abdallah Hassan, Nicholas Mejah, Fred Nkata,David King’atia na kipa mkali Farouk Shinalo ambaye majuzi ameitwa kaika kikosi cha taifa Harambee Stars kwa fainali za AFCON kule Misri.

Safu ya ufundi inaongozwa na kocha mkuu Mwalala ambaye ameunda kikosi thabiti na cha nidhamu.Anasaidiwa na mkufunzi mdogo Nasoro Mwakoba anayetoka sehemu za Ng’ombeni Digo sambamba na mkufunzi wa magolikipa Razak Siwa.

Siwa alokuwa kipa mahiri amemjenga na kumnowa Shinalo na kuwa kipa bora anayeruka na kunyaka matobwe moto moto kama zee la nyani!.

Kwa sifa hizi Bandari sharti ilenge juu na kuleta ushindi kwani wapwani wana njaa na kiu ya kumtaka yule mwanamwali ambaye mara ya mwisho ni wakati timu ya Feisal ilipomleta kwa kuwa bingwa Kenya.

Je, Bandari itafanya hivyo na kumtowa mwanamwali bara hadi mwambao bahari kuu?.Ndio yawezekana ! chembelecho Barack Obama kazi kwenu wanakwetu!.                           

Man-U na PSG wampigania Sancho

Viabu viwili vya soka vikubwa Ulaya Man-U na Paris Saint Germain wanamng’ang’ania mchezaji Janon Sancho wa Borussia Dortmund ya Ujerumani.

Sancho barobaro wa miaka 18 raia wa Uingereza hivi sasa yuko katika darubini kali ya vilabu hivi viwili ambavyo vina uwezo mkubwa wa pesa zinazo vunja milima na majabali.

Mchezaji huyu mahiri anayecheza sehemu ya pembeni yaani winga ni moto wa kuotea mbali na ametowa mchango mkubwa kwa timu yake ya Dortmund.

Sancho ni mwepesi, jasiri,mjanja, mwenye kujiamini wa chenga za maudhi mbali nakuwa na tajriba nyeti ya nidhamu ndani na nje ya uga.

Habari zengine kutoka Old Trafford ni kwamba kuna habari ya kukarabati kikosi kizima cha Man-U kwa kuwaleta wachezaji wapya kutia jeki timu.

Duru zatueleza kwamba Man-U imetenga dola milioni 155 za Uingereza kuwanasa wachezaji wawili wa kimataifa wa Ureno.

Wareno hao walio katika rada kali ya Old Trafford ni beki matata hapiti mtu hapa  Ruben Dias na wa kiungo cha kati tena mshambulizi Joao Felix.

Bwenyenye wa New Castle mbioni kuuza klabu

Bwenyenye Mike Ashley mmiliki wa New Castle United ya ligi kuu ya Uingereza EPL anahangaika kutafuta tajiri wa kununua klabu hiyo ya kale.      

Bwana huyu amesinywa na matokeo mabovu ya timu yake kwani imekuwa gunia la kubebeshwa magoli.Matokeo haya yameleta hasara kubwa ya mapato ikichukuliwa kuwa ngozi katika karne hii ni kitegea uchumi na hvyo biashara kubwa.

Ashley tayari amewasiliana na mabwenyenye wenye ngwechere sufufu kama mchanga wa bichi.Mdaku wetu atueleza kuwa kuna mabwenyenye takriban sita wa kiarabu kutoka Qatari na falme za kiarabu wanaotafakari kumiliki kilabu hicho.

Mmoja wa mabwenyenye hawa ni Al-Mansor El- ibn Masuud-El- Khantosoh mwenye tumbo kubwa kama karai na madevu marefu kama kuti la mnazi!

El-Khantoosh ana wake wanne warembo na watoto 38 ana visima 200 vya mafuta, ndege 50, meli 160 na makampuni makubwa kote ulimwenguni.

Al-Mansur hivi sasa anashauriana na mawakili wake kuhusu hatua ya kuchukuwa kama atatoboka mabilioni na kusikizana na Ashley ama kupuuzilia mbali mradi huu.

By Mose Sammy 2 hrs ago
Golf
Over 180 golfers to grace Mulembe tournament
By Ben Ahenda 8 hrs ago
Rugby
Cheetahs start training ahead of Super Series
Athletics
All set for Ghetto Marathon
Athletics
Kirui, Kibiwott to renew rivalry at Kip Keino Classic