Jubilee yadinda kuunga mkono Khalwalwe kuwania ugavana

 

Huku hamahama za chama zikizidi kupamba moto miongoni mwa “viongozi watarajiwa” sehemu mbalimbali nchini, wagombea wamekuwa wakikesha usiku kucha na kuweka mikakati thabiti zitakazo hakikisha wanawania na kuibuka washindi katika viti kadhaa serikalini. Majuma kadhaa yaliyopita,  tulimshuhudia aliyekuwa seneta wa Kakamega Bonny Khalwale akikigura chama cha Ford Kenya na kutangaza hadharani kumuunga mkono naibu rais William Ruto katika azimio lake la kuwania urais kwa uchaguzi mkuu ujao.

Hii ni kwa lengo la wanachama wa Jubilee kumuunga mkono pia na kuhakikisha amekitwa kiti cha ugavana kaunti hiyo ambayo amekuwa akimezea mate kwa zaidi ya mwongo mmoja sasa. Hata hivyo huenda ndoto zake zikazikwa kwa kaburi la sahau kutokana na viongozi wa chama hicho ukanda huu wa Magharibi kujitenga na fununu za kumuunga mkono kama gavana kwa uchaguzi mkuu ujao huku wakisema wakati ukifika watamteua yule watakaye pendekeza kuipeperusha bendera hiyo.

Wakiongozwa na mwenyekiti wao Moses Lumiti wanachama hao wamepuzilia mbali uvumi unaoenezwa na baadhi ya wanasiasa kuwa wao kama chama wametangaza kumuunga mkono Khalwale wakidai hawajapendekeza yeyote kuwania kiti hicho na uamuzi wao wakumkaribisha chamani hakina uhusiano wowote na kumuunga mkono.

“Kwa sisi kumruhusu khalwale kujiunga na sisi haimanishi ametakazwa kuwania ugavana katika chama chetu,” alisema Moses. Aidha wamesema wao kama wasimamizi wa chama katika kaunti ya Kakamega, wakati ukifika watampendekeza yule atakaye peperusha bendera ya chama hicho Katika nyadhfa mbalimbali. “Chama kina sheria yake ambayo lazma ifwatwe. Ikifika wakati tutakaa chini judaliane na tuone tutawaunga akina nani mkono, kwa sisi kumkaribisha katika chama haimanishi tumemtakaza kupeperusha bendera hiyo,” alisema Moses.     

 Kwa upande mwingine wamekiri kuunga mkono mwafaka wa mapatano baina ya rais Uhuru Kenyatta na kinara wa upinzani Raila Odinga na kumtaka rais kuwa mwangalifu haswa kwa wale wanaoruhusiwa kujiunga na chama chao. “Hatupingi mwafaka wa rais Uhuru Kenyatta na Raila, ni ukweli imezaa matunda lakini watu ambao wanaruhusiwa kuingia kwa chama ndio tuna shida na wao, wengine nia yao ni kuisambaratisha chama,” alisema Welimo. Haya yanajiri huku viongozi wa kidini kutoka ukanda huu wakitoa wito kwa rais Uhuru Kenyatta, pamoja na viongozi wakuu katika chama hicho kutafuta suluhu kuhusu misururu ya migogoro inayoikumba chama hicho huku dalili za kutemwa nje kwa naibu wa rais William Ruto ifikapo mwaka wa 2022 zikijidhihirisha peupe.