Kampuni za mawasiliano zakadiria hasara

Na, Suleiman Yeri/Beatrice Maganga
Kampuni za mawasiliano zakadiria hasara
Kampuni za mawasiliano nchini zimepata hasara ya takriban shilingi miioni 280 kufuatia uharibifu wa mitambo yake. Mamlaka ya Mawasiliano nchini, CA imesema uharibifu umechangiwa na visa vya ugaidi na ghasia za kisiasa, msimu wa uchaguzi.
Akizungumza na wanahabari, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya hiyo, CA Francis Wangusi amevishtumu visa vya kuharibiwa kwa minara ya mawasiliano akisema vinawasababishia wawekezaji hasara ya mamilioni ya fedha hautaruhusiwa.
Kauli yake imejiri siku chache baada ya wafuasi wa Muungano wa NASA kudaiwa kuiharibu mitambo ya mawasiliano ya Kampuni ya Safaricom kwa ghadhabu baada ya Mahakama ya Juu kudumisha ushindi wa Rais Mteule, Uhuru Kenyatta.
Wangusi amesema hatua hiyo imeathiri huduma za mawasiliano eneo hilo. Aidha ameongeza kuwa kuharibu mitambo ya mawasiliano kwa maksudi hakufai na kuwashauri Wakenya kuwa waangalifu kabla ya kuchukua hatua kama hizo kwani mawasiliano husaidia pakubwa wakati wa matukio ya dharura.
Ikumbukwe Kampuni ya Safaricom ni miongoni mwa zile ambazo NASA iliwataka wafuasi wake kususia bidhaa zake na huduma huku ikiahidi kutoa orodha nyingine ya bidhaa za kususiwa kufikia mwishoni mwa wiki hii.
Afisa Mkuu Mtendaji wa NASA, Norman Magaya anasema Kamati ya Vuguvugu la Upinzani (National Resistance Movement Commitee) itatoa orodha nyingine ya kampuni hizo ambazo wanadai zinainufaisha serikali ya Jubilee na kuiwezesha kusalia uongozini.
Kauli ya Magaya imetiliwa mkazo na Mwenyekiti wa ODM, John Mbadi ambaye anasema wataendelea kuchunguza kampuni ambazo kwa njia moja au nyingine zilitatiza uchaguzi wa urais wa Agosti 8, ambapo Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi kabla ya Mahakama ya Juu kufutilia mbali matokeo hayo.
Ikumbukwe kuwa tayari NASA imezitaja kampuni za Bidco, Safaricom na Brookside na kuwataka wafuasi wake kususia bidhaa na huduma za kampuni hizo.?

Related Topics