Chebukati apinga wito wa kujiuzulu

Na, Beatrice Maganga
Chebukati apinga wito wa kujiuzulu
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, IEBC Wafula Chebukati amepuuza shikizo la kumtaka yeye na makamishna wengine wa tume wajiuzulu. Shinikizo hilo la hivi punde limetolewa na Afisa Mkuu Mtendaji wa Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinadam, KHRC, George Kegoro. Chebukati ambaye amezungumza kwa mara ya kwanza tangu Mahakama ya Juu idumishe ushindi wa Rais Mteule, Uhuru Kenyatta amesema makamishna wa IEBC wako ofisini kihalali. Kegoro anasema kuwa Chebukati anastahili kuandaa mpango wa kuhakikisha wanaondoka ili kufanikisha mabadiliko muhimu katika IEBC.
Ikumbukwe kabla ya marudio ya uchaguzi wa urais, Chebukati aliashiria kwamba huenda angejiuzulu iwapo masharti fulani yasingetimizwa kukiwamo kukomeshwa kwa mwingilioni wa wanasiasa katika shughuli za tume yake. Hata hivyo kabla na baada ya marudio ya uchaguzi wa urais Oktoba 26, alisema vizingiti dhidi ya uchaguzi huru na haki vilikuwa vimeondolewa. Kuhusu uamuzi wa Mahakama ya Juu, Chebukati amesema IEBC inasubiri uamuzi kamili wa mahakama hiyo ili kutathmini mapendekezo yake. Aidha ameipongeza tume hiyo kwa kuandaa chaguzi mbili za urais kwa kipindi cha miezi mitatu.
Pindi uamuzi wa kuzitupilia mbali kesi zilizowasilishwa kutaka kubatilishwa kwa marudio ya uchaguzi wa urais Oktoba 26 IEBC kupitia mtandao wake wa Twitter ilipongeza uamuzi huo ikisema ni ishara kwamba tume ilizingatia maandalizi ya uchaguzi huo kwa njia huru na ya haki.

Related Topics