Zaidi ya wasichana 20,000 hupachikwa mimba kila mwaka katika kaunti ya Kakamega asilimia kubwa wakiwa wamo chini ya miaka 16. Haya ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na shirika la AMREF kaunti hiyo ambapo ilibainika, Kakamega imo miongoni mwa kaunti tano nchini zinazoandikisha idadi ya juu ya wasichana wanaopachikwa mimba. Kaunti zingine ni Nairobi, Kilifi, Bungoma na Nakuru. Kulingana na Sylvia Wamugi (Afisa msimamizi wa AMREF Kakamega) zaidi ya wasichana 50 hupachikwa mimba kila siku kaunti hiyo huku maeneo bunge ya Shinyalu, Matungu na Malava yakiwa kati ya maeneo ambayo yanaongoza kwa visa hivyo.
Kando na upachikaji wa mimba, jinsia ya kike pia imo katika hatari ya kudhulumiwa kimapenzi ikiwemo kubakwa, kunajisiwa pamoja na kuozwa wakiwa na umri mdogo kinaya ikiwa jamaa waliojukumiwa kuwalinda na kuwakuza wakitajwa miongoni mwa wanaoendeleza dhulma dhidi yao na kuhatarisha kizazi kijacho. Kwa kipindi chini ya mwezi mmoja zaidi ya visa 10 vya dhulma kwa wanafunzi wasichana vimeripotiwa kaunti hii nyingi zikihusishwa na jamaa wa karibu huku waathiriwa wakikosa kupata haki nao washukiwa wakikosa kuchukuliwa hatua zozote zile.