Rais Kenyatta azungumzia uwezekano wa kuifanyia katiba marekebisho

Rais Uhuru Kenyatta leo hii ameongoza sherehe ya 57 ya siku ya Madaraka huku akitumia maadhimisho hayo kuzungumzia uwezekano wa kuifanyika katiba marekebisho. Rais Kenyatta amesema lengo si kuondoa yaliyoko bali kuiboresha zaidi katiba iliyoidhinishwa mwaka 2010.

Rais amesema Kenya inahitaji mageuzi ya katiba ambayo yatakomesha ghasia kila wakati wa uchaguzi ambazo zimekuwa zikishuhudiwa nchini tangu mwaka wa elfu moja mia tisa tisini na mbili, kuimarisha demokrasia na kudumisha umoja wa wananchi. Ikumbukwe Rais Kenyatta na Kinara wa ODM, Rauka Odinga wamekuwa wakiendeleza mchakato wa kuifanyika katiba marekebisho kupita Mpango wa Upatanisho, BBI.

Rais Kenyatta aidha amepigia debe ufanisi ambao umeshuhudiwa nchini kwa kipindi cha miaka saba ya utawala wake akisema kufikia sasa serikali yake imefanikiwa kujenga takriban kilomita elfu moja za barabara kila mwaka, hali ambayo ameitaja kuwa  hatua kuu kutoka nyakati za ukoloni ambapo Kenya ilikuwa na kilomita elfu moja mia nane pekee za barabaraza zilizotiwa lami. 

Vilevile ameutaja ujio wa Reli ya Kisasa nchini, SGR kuwa miongoni mwa mambo ya kujivunia chini ya utawala wake. Aidha ametangaza kufanikiwa kutimiza baadhi ya maazimio yaliyokuwa ya waanzilishi wa taifa kukiwamo utoaji wa hatimiliki za ardhi takriban milioni 4.5.

Ikiwa miaka 57 ya Madaraka, Rais Kenyatta amewahimiza viongozi kuendelea kuwahudumia wananchi kwa uadilifu akisema viongozi wanaofaa ni wale wanaofanya kipaumbe maslahi ya wananchi wala si wenye kujitakia makuu binafsi.

 

Related Topics

katiba uhuru