Serikali yaweka marufuku ya kutoka na kuingia kwenye kaunti nne nchini

Serikali imetangaza marufuku ya kutoka na kuingia kwenye Kaunti za Nairobi, Mombasa, Kilifi na Kwale, kwa muda wa siku ishirini na moja.

Katika tangazo hilo, serikali aidha imesema kuwa marufuku hayo yataanza kutekelezwa leo saa moja usiku kwenye Kaunti ya Nairobi.

Kinyume na ilivyoeelewaka awali, marufuku hayo hayataathiri shughuli za uchukuzi wa ndani kwa ndani kwenye kaunti hizo kwa kuwa wakazi wataruhusiwa kusafiri kutoka eneo moja hadi jingine ndani ya kaunti hizo.

Katika hotuba yake, Rais Uhuru Kenyatta amesema kuwa marufuku hayo yatayaathiri maeneo kadhaa yanayopakana na Jijini la Nairobi yakiwamo Rironi, Kiambu Mjini, Athi River, Ongata Rongai, Kiseriani, Kitengela miongoni mwa maeneo mengine yatakayoathirika.

Aidha kwenye kaunti za Kilifi, Mombasa na Kwale, agizo hilo litaanza kutekelezwa kuanzia Jumatano wiki hii. Kwa mujibu wa Kenyatta, wakazi wataruhusiwa kusafiri japo ndani ya maeneo ya kaunti hizo.

Kuhusu magari yanayosafirisha mizigo vilevile vyakula, Rais Kenyatta amesema yataruhusiwa kusafiri kutoka kaunti moja hadi nyingine japo, kwa kuzingatia masharti ya kuwa na dereva mmoja, na wasaidizi wasiozidi watatu vilevile kuhakikisha wanawasiliana na mamlaka husika.

Hata hivyo , amesema amri ya kutokuwa nje kuanza saa moja usiku hadi saa kumi na moja alfajiri itaendelea kutekelezwa.

Ikumbukwe mikakati hii ya ziada imechukuliwa baada ya awali serikali kuafikia uamuzi huo, ili kudhibiti kuendelea kusambaa kwa virusi vya korona nchini.

Awali serikali iliwaagiza wahudumu wa magari ya uchukuzi wa umma, kuhakikisha kuwa wanaweka kemikali za kuua viini kwa abiria, kudumisha umbali wa mita moja baina yao, kwa kubeba asilimia sitini ya abiria.