Uwezekano wa kuwa MRC ‘A’ na ‘B’

Viongozi wa MRC wakihutubia wananchi. [Picha: Pambazuko]

Hali inabashiria kwamba huenda kukawa na makundi mawili yanayoorodheshwa kuwa ya MRC lakini likawa moja la kundi ‘A’ likawa lile rasmi la kina Omar Mwamnuadzi na lingine la ‘B’ ambalo uhai wake ni wa kusadikika tu kufuatia matukio sawa ya uvamizi wa vijana ulioripotiwa juzi na idara ya polisi katika kaunti ya Kilifi.

Muda mfupi tu baada ya taarifa za vijana wanaosemekana walikuwa wanachama wa kundi la MRC kuponyea chupu kwenye msitu wa Jibana ambapo kulingana na taarifa za polisi, ilibainiwa kuwa zaidi ya vijana 50, Pambazuko ilijaribu kuchimba uwezekano huo kutaka kujua kutoka kwa baadhi ya viongozi wake lakini wakakana vikali kwamba vijana hao kamwe hana uhusiano wowote na MRC ambayo inaangazia haki yake kisheria.

MRC ‘B’ Kulingana na taarifa za polisi, wanasema kwamba mwamko mpya wa kundi hili la MRC umeanza kushuhudiwa katika mwambao wa pwani ikiwa ni baada ya vijana zaidi ya 50 kuvamiwa ndani ya msitu wa Kaya Jibana wakidaia kwenye zoezi la kula kiapo. Polisi hao wanakadiria umri wa vijana kuwa kati ya miaka 25 had 35.

 Polisi wakiongozwa na mkuu wao wa jimbo la Kaloleni, Kennedy Osando, wanasema walivamia msitu huo na kuwakuta vijana wakiwa kwenye harakati zao za viapo. “Tuliwarai wajisalimishe lakini walikataa hivyo tukawafyatulia risasi. Tunao uhakika kwamba wengi wao walipata majeraha,” atushangaza mkuu huyu wa polisi. Hadi kufikia hapo, wadadisi wa masuala ya ndani wanadai kwamba polisi bado hawajatuambia kitu cha kunyooka kuhusu ukweli wa kisa

hiki. Itakuaje umimine risasi kikundi cha watu hamsini waliokusanyika pamoja na usipate jeruhi hata mmoja ila ufikirie kuwaambia wandishi habari kwamba huenda wengi wamejeruhiwa baada ya kudinda kujisalimisha? Mauaji ya vijana 2012 Mnamo mwezi Septemba tarehe 27, mwaka 2012 miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa 2013, zaidi ya watu 11 akiwemo mzee wa mtaa waliauawa katika kijiji cha Tsangatsini kilichoko eneo la Kaloleni, kaunti ya Kilifi.

Miongoni mwa vijana hawa walitokea sehemu tofauti za pwani lakini wengi wakichomozea kaunti ya Kwale na Mombasa. Na  kweli wakati huu, kundi la MRC lilikuwa ni moto wa kuotea mbali na kamwe haingewezekana kudadisi kwamba kisa cha aina hii, kilitokana na upande upi, aidha wa vuguvugu la MRC ama kundi lingine ambalo liliundwa wakati huo la “Pwani ni Kenya” ambalo lilifadhiliwa na mkono wa serikali dhidi la lile la MRC la “Pwani si Kenya”.

 Hapa kungali kuna swali gumu kwa sababu, wachunguzi waliofuatilia kisa cha Tsangatsini, walichimba makubwa kuhusiana na kuhusikakwa vijana waliouawa na wengine waliotumia mguu ni ponye kupona.

MRC wakati huo walidinda kuhusika na tukio hilo ama kuwa na ushirikiano na vijana waliohusika. Mamluki wa MRC Tulipofuatilia chanzo cha kisa cha Tsangatsini cha Septemba 2012, tuliwahi hata kuhudhuria baadhi ya mazishi ya vijana waliouawa na kuchimba kwa kina mienendo yao na mawasiliano yao na wazazi wao siku chache kabla ya tukio hilo. Kwanza kabla ya kisa cha kijiji cha Tsangatsini, eneo la Kaloleni cha Septemba 27, 2012, vijana hao walishiriki kwenye tukio ama kisa kingine cha uvamizi wa afisa wa polisi katika eneo la Dzombo lililoko Lunga Lunga, kaunti ya Kwale kwa kumkata kichwa polisi mnamo Septemba 13.

Baada ya tukio hili, vijana hao walitimuliwa kwa kuvamiwa na wananchi pamoja na maafisa polisi huku wengine wakitorokea Mombasa na makwao, wengine wakiwa ni kutoka kilomita chache kutoka Dzombo kabla ya kulipwa tena kuelekea Tsangatsini. Kulingana na ushahidi wa awali kuhusiana na kisa hicho, vijana wengi waliohusishwa hawakuwa wanachama wa MRC bali walikuwa Mamluki waliokodishwa kwa kudanganywa na watu fulani (yaaminika wanaisasa wa pwani waliokuwa wana hofu ya kutatizika kisiasa katika uchaguzi mkuu wa 2012/13) ikidaiwa waliokuwa una ukaribu wa kusaidia serikali kuzima wimbi la MRC.

 Jamaa na marafiki wa vijana hawa wanasema walikuwa wafanya biashara wa reja reja katika barabara za mji wa Mombasa hususan wachuuzi wa njugu, mifuko, mitumba, na kadhalika katika barabara za Digo Road, Biashara Street, Mwembe Tayari na kadhalika wengi wakitoka Kwale na Kilifi. Katika kila kazi ya uvamizi, kila mmoja alilipwa shilingi 40,000 kumwachia mkewe ama mama yake nyumbani.

Mazoezi ya jinsi ya kutumia silaha na maagizo maalum  kuhusiana na kazi yao hiyo ya umamluki, yalifanyika katika sehemu maalum za kisiwani Mombasa kabla ya kuhitimu kuorodheshwa safarini. Kazi kubwa kwao, ni kutiwa mori na kuhakikishiwa kwamba, maslahi yao ya nyumbani yangetekelezwa.

“Kabla ya mtoto wangu kuawa kule Tsangatsini, alikuja mwendo wa usiku wa manane mnamo Septemba 14, 2012 akiniambia mama nimekupitia chukua hizi shilingi 20,000 lakini kesho asubuhi naelekea kukomboa pwani yetu,” asimulia mzazi mmoja kutoka kijiji cha Mgombezi, ambacho kilishuhudia kuzikwa vijana wawili. Mama anashangaa kwamba baada ya kisa cha Tsangatsini, aligutuka kusikia kwamba kati ya waliouawa ni mtoto wake ambaye alikuwa ameoa miezi michache iliyopita kabla ya mauti yake. Alikuwa ni mchuuzi wa nguo za mitumba katika barabara ya Biashara Street.

Sauti ya MRC Kulingana na Pastor Nyae Ngao ambaye ambaye ni mwanachama wa MRC na mhubiri wa kanisa anasema kwamba kutokana na umakini wao na jinsi wanavyoyii sheria kamwe haoni kana kwamba vijana hao 50 wanaodaiwa kuvamiwa msitu wa Jibana juzi kuwa ni wafuasi wa kundi hili. Anasema kuwa uwezo wa serikali kutumia Mamluki upo na anasikitishwa na baadhi ya vijana kwamba wanajishusha daraja la maisha kwa kukubali kutumika kwa mipango kama hiyo. Pasta Nyae pia anakumbuka kisa cha Tsangatsini na vinginevyo kama sampuli ya magenge ya mamluki ambao hukodishwa ili kuharibia hadhi MRC.

 Anasema serikali imekuwa na njama nyingi tangu 2013 wakati MRC iliposhtaki tume ya IEBC kuhusiana na mipaka. Anashuku kwamba kuazrika kwa kesi hii na kucheleweshwa kwa kusikizwa kwake ndicho chanzo cha serikali na mahakama kushikwa na mzizimo wa hofu kuhusiana na suala la mipaka.