Zaidi ya asilimia 70 ya walimu wahudhuria mafunzo ya mtalaa mpya, Mombasa

Asilimia 70 ya walimu kwenye Kaunti ya Mombasa wanahudhuria mafunzo ya mtaala mpya wa elimu 2-6-3-3-3 ambayo yanaendelezwa kwenye shule mbalimbali za msingi Jijini humo.

Afisa mkuu wa mtalaa huo Curriculum Support Officer ( CSO ) eneo la Ziwani Zainab Ali amesema kwamba idadi hiyo imechangiwa na walimu kufahamu umuhimu wa mafunzo hayo.

Akizungumzia suala la pingamizi kutoka kwa viongozi wa Chama cha Kitaifa cha Walimu, KNUT kuhusu mtaala huo, Zainab haoni haja ya pingamizi hilo ikizingatiwa kwamba Wizara ya elimu inajukumika kuhakikisha inaiboresha sekta ya elimu.

Kauli yake inajiri saa chache baada ya Waziri wa Elimu Profesa. George Magoha kusisitiza kwamba mafunzo ya mtaala huo yataendelezwa kama yalivyopangwa licha ya pingamizi kutoka kwa viongozi wa KNUT.

Akizungumza alipozuru shule ya msingi ya Ronald Ngala jijini Mombasa ambako mafunzo hayo yanaendelea, Magoha badala yake amesema kwamba hatalegeza kamba katika malengo yake ya kuiimarisha sekta ya elimu.

Hayo yanajiri huku Katibu Mkuu wa KNUT Wilson Sossion akishikilia kauli yake kwamba walimu hawataunga mkono utekelezwaji wa mtaala huo wa 2-6-3-3-3.

Kulingana na Sossion, walimu zaidi wanapaswa kuajiriwa, kuboreshwa kwa miundo msingi sawa na walimu kupewa muda wa mafunzo huku akiongeza kwamba utekelezwaji wa mtaala huo uliaharakibwa bila kuhusishwa kwa washikadau wote katika sekta ya elimu.

Related Topics