Swazuri na wenzake kusalia korokoroni hadi Jumanne

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi, NLC Muhammad Swazuri na maafisa wengi kumi wa Tume hiyo watasalia rumande hadi Jumanne wiki ijayo kutokana na likizo ndefu ya pasaka.

Maafisa hao wamefikishwa mahakamani mapema leo wakikabilia ma mashtaka mbalimbali ikiwemo utumizi mbaya wa mamlaka na ufujaji wa fedha za umma.

Mahakama ya kukabili ufisadi imeamuru kuwa kumi na mmoja hao waendele kuzuiliwa huku wakisubiri uamuzi wa ombi lao la kuwachiliwa kwa dhamana.

Swazuri alikamatwa jana kufuatia madai ya ulaghai na utumizi mbaya wa mamlaka wakati alipolipa fidia kwa Kampuni kwa jina la Tornado Carriers Limited ambayo ardhi yake ilitwaaliwa kwa lazima na serikali mwaka 2017 wakati wa ujenzi wa baabara ya Mombasa Southern Bypass na ya Kipevu Oktoba mwaka 2013.

Mara ya kwanza ardhi hiyo ilifaa kulipiwa shilingi milioni 34 kiwango ambacho kilikataliwa kabla ya Swazuri kuagiza tathmini ifanywe upya huku kiwango cha pili kikifikia shilingi milioni 109 fedha zilizotolewa na Mamlaka ya Barabara Kuu.

Hata hivyo, Tornado Carriers ililipewa shilingi milioni 54 huku shilingi nyingine milioni 54 zikilipwa kampuni ya uwakili.