Pendekezo la kuondoa kesi dhidi ya majaji wanne wa Mahakama ya Juu la wasilishwa

Mohammed Mohamud Sheikh, mmoja wa waliowasilisha kesi kuondolewa kwa majaji wanne katika Mahakama ya Juu kufuatia tuhuma za ufisadi, sasa anapendekeza kuondolewa kwa kesi hiyo.

Sheikh anasema angependa kutupilia mbali ombi hilo na kwamba hajashinikizwa na yeyote bali amefanya hivyo mwenyewe.

Hata hivyo huenda ombili lake halitatiliwa mkazo hasa ikizingatiwa aliwasilisha kesi hiyo akiwa na watu wengine.

Wiki iliyopita Tume ya Huduma za Mahakama, JSC ilithibitisha kupokea ombi la kutaka kuondolewa kwa majaji Mohammed Ibrahim, Jackton Ojwang, Smokin Wanjala na Njoki Ndung'u kwa kosa la kutoa uamuzi usio wa haki, hali iliyosababisha kudumishwa kwa ushindi wa Gavana wa Wajir, Mohamed Abdi Mahamud.

Hapo jana Jaji Njoki Ndung'u alitaka Idara ya Upelelezi, DCI kumchunguza yeye pamoja na majaji wengine wa mahakama hiyo kufuatia madai ya ufisadi.

Ndung'u ambaye anashikilia kwamba hakusika na sakata hiyo, anazitaka idara za uchunguzi kuharakisha hasa ikizingatiwa tayari Tume ya Huduma za Mahakama, JSC inaendeleza uchunguzi huo.

Jaji Ndung'u anataka DCI kuchunguza iwapo kulikuwapo mawasiliano kati yao na watu ambao wametajwa kwenye sakata hiyo. Majaji hao wanashtumiwa kupokea hongo ili kutoa uamuzi usio wa haki ili kudumisha ushindi wa gavana Mahamud.

 

Related Topics