Serikali yalaumiwa pakubwa kufuatia uhaba wa chakula kwenye kaunti 13.

Serikali imelaumiwa kufuatia uhaba wa chakula kwenye kaunti 13 ambazo zinakumbwa na ukame nchini. Baadhi ya wabunge wakiongozwa na Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa, John Mbadi aidha wamewasuta maafisa wa Mamlaka ya Kukabili Majanga Nchini kwa kudai kwamba hakuna watu ambao wameaga dunia kutokana na makali ya njaa.

Wakizungumza kwenye vikao vya Jumanne alasiri, wabunge hao aidha wameitaka serikali kuhakikisha wanawasambazia waathiriwa vyakula vingine kando na mahindi.

Wakati uo huo, Kiranja wa Wengi katika bunge hilo, Benjamin Washiali amewalaumu magavana kwa kutochukua hatua za dharura hata baada ya idara ya utabiri wa hali ya anga kutangaza kwamba kutashuhudiwa hali ya kiangazi kwenye baadhi ya maeneo nchini.

Ikumbukwe Mkuu wa Mamlaka ya Kukabili Majanga, James Oduor alisema taarifa zinazotolewa zinapotosha umma kwani hakuna mtu aliyefariki kutokana na ukame.

Aidha, Naibu wa Rais, William Ruto alisema tayari serikali imetenga shilingi bilioni mbili fedha za dharura ili kukabili ukame kwenye maeneo hayo.

Related Topics

Uhaba wa Chakula