COTU, yapewa muda wa kusuluhisha mvutano kati yao na serikali nje ya mahakama.

Mahakama ya Uajiri na Leba imeongeza muda wa kuzuia kutekelezwa kwa mpango wa serikali kuwatoza waajiriwa asilimia 1.5 ya mishahara yao ili kufanikisha ujenzi wa makazi ya bei nafuu. Jaji Hellen Wasiswa hata hivyo ameupa upande wa mlalamishi ukiongozwa na Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi, COTU, muda wa kusuluhisha mvutano huo na serikali nje ya mahakama.

Suala hilo litarejelewa mahakamani tarehe 18 Aprili ambapo wahusika watatakiwa kueleza hatua walizopiga katika kutatua mvutano huo. Katika kesi yake, Katibu Mkuu wa COTU, Francis Atwoli aliibua suala la kutohusishwa kwa Wakenya katika kuamua kadhalika kutozingatia kwamba kuwatoza Wakenya asilimia 1.5 ni sawa na kuwapunguzia mshahara.

Mapema mwaka huu, Waziri wa Uchukuzi na Miundo-msingi alidokeza kwamba tayari ulikuwapo mwafaka kuhusu suala hilo japo hilo halijadhirika hadi sasa. Katika mpango wenyewe, waajiriwa watatozwa katia ya shilingi 200 na 2500 huku serikali ikilenga shilingi bilioni 48.

Serikali imefafanua kwamba fedha zinazotozwa zitahesabiwa kuwapo malipo ya uzeeni kwa wale ambao hatimaye hawatahitaji makazi ya bei nafuu.

Related Topics