Shule ya Wavulana ya Njoro, Nakuru yafungwa ghafla

Shule ya Wavulana ya upili ya Njoro kwenye Kaunti ya Nakuru imefungwa ghafla. Maafisa wa Elimu kwenye kaunti hiyo ya Nakuru walichukuwa hatua hiyo baada ya Mwalimu kugundua kuwa kulikuwa na petroli kwenye bweni moja ya shule hiyo inayotumiwa na zaidi ya  Wanafunzi 70.

Haya yanajiri siku chache, baada ya bweni nyingine kuteketezwa na mali yenye dhamani isiyojulikana kuteketea. Wanafunzi wote walitumwa nyumbani baada ya maafisa wa Elimu, Usimamizi wa Shule na Maafisa wa usalama kufanya mkutano na kuafikia uamuzi huo.

Mkurugenzi wa Elimu eneo la Bonde la ufa Mary Gaturu, amesema uchunguzi umeanzishwa ili kubaini jinsi petroli hiyo ilivyofikishwa ndani ya shule hiyo. Jumamosi usiku inasemekana kuwa kuna mtu aliyeimwaga katika bweni ya wanafunzi huku ikishukiwa kuwa huenda ni mwanafunzi .

Maafisa wa Upelelezi kutoka Njoro wakikishirikiana na  Maafisa wa polisi ,walifika kwenye shule hiyo kuendeleza uchunguzi huku wakisema huenda wanafunzi hao walihusika katika visa hivyo, baada ya  kulalamikia muda wa masomo kuongezwa.