Mzazi azuiliwa katika kituo cha polisi kwa kukaidi agizo la serikali

Mwanamume mmoja kutoka eneo la Matuga kaunti ya Kwale alilazimika kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Kwale baada ya kukaidi agizo la serikali la kuwapeleka watoto wake shuleni na hospitali kwa madai ya msimamo mkali wa dini yake.

Tumaini Hamisi anayeshiriki katika kanisa la Good News International huko Likoni alishikilia kuwa dhehebu lake haliruhusu mshirika kupata elimu wala kuenda hospitalini kutafuta matibabu hasa wanapokuwa wagonjwa.

Hamisi aidha alisema kulingana na imani ya dhehebu hilo, suala la elimu siyo jambo la muhimu kwani baadhi ya watu waliosomo wamesalia kuhangaika hali iliyompelekea kuwaficha wanawe wawili waliostahili kwenda shuleni.

"Elimu ni ya shetani kwani unahitaji roho mtakatifu kusoma biblia pasi na kwenda shuleni ama hospitali kutibiwa si mpango wa Mungu bali unahitaji kuwa na imani," alisema Hamisi.

Kwa upande wake mama wa watoto hao Kache Nyawa aliyepewa talaka na mume wake baada ya kuasi imani ya dhehebu hilo alieleza kushangazwa na hatua ya mumewe huku akishikilia kwamba ni sharti wanawe wapate elimu.

"Shida yangu ni kuwaona watoto wangu wala sina haja na mume wangu ambaye tuliwachana kitambo licha ya kuniambia aliwaacha watoto nyumbani bado sijawaona. Hao watoto wanajua kwa babu yao wangeenda huko lakini nilipomuuliza baba yangu aliniambia hajawaona watoto kwa muda wa siku mbili," alieleza Nyawa.

Hata hivyo OCPD wa eneo la Matuga Joel Chesire alitoa onyo kwa wazazi watakaokiuka agizo la serikali la kuwapeleka watoto wao shuleni huku akisema kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

"Natoa onyo kwa wafuasi wa kanisa hilo kama mko na watoto ambao wako nyumbani wapeleke shule kabla hatujawafikia. Sheria iko wazi licha ya serikali kutoa elimu na matibabu ya bure, hakuna sababu ya wananchi kujificha kanisani kwa kisingizio kwamba dini yao hairuhusu mambo kama hayo," alisema Chesire.