Rais wa Sudan Omar Al Bashir aivunja serikali

Wasiwasi umetanda nchini Sudan baada ya Rais wa taifa hilo Omar Al Bashir kutangaza hali ya hatari na kuivunja serikali na kuwafuta kazi magava wote. Bashir alitoa tangazo hilo kupitia runinga za taifa hilo na kuwateua maafisa wa usalama kuchukua nafasi ya magavana hao. Katika siku za hivi karibuni maandamano yamekuwa yakiendelea nchini humo huku wanaopinga uongozi wake wakimtaka uondoka madarakani.

Hata hivyo katika taarifa yake, Bashir aliyataja maandamano hayo kuwa yanayolenga kutatiza ustawi wa nchi hivyo kutangaza hali ya hatari itakayodumu kwa kipindi cha mwaka mmoja. Vilevile alilitaka bunge la nchi hiyo kusitisha mabadiliko yoyote ya katiba ambayo yangeongeza muda wake wa kuhudumu.

Chanzo cha maandamano ya hivi punde nchini humo ilikuwa kuongezwa kwa bei ya mkate na mafuta mwezi Disemba lakini mambo yakabadilika huku waandamanaji wakipinga utawala wake kwa kipindi cha miaka thelathini sasa.

Tangu maandamano hayo yaanze inaarifiwa zaidi ya watu elfu moja wamekamatwa na wengine kuuliwa kwenye makabiliano na maafisa wa usalama.