Vikao vya bunge vyarejelea huku uteuzi wa wanakamati za shughuli za bunge ukijadiliwa

Hatimaye vikao vya bunge vimerejelea leo hii kwa mara ya kwanza mwaka huu huku jukumu la kwanza likiwa kujadili uteuzi wa watakaokuwa wanachama wa kamati za shughuli za bunge katika Bunge la Kitaifa, vilevile la Seneti. Aidha masuala ya mgomo wa wauguzi na matatizo katika sekta ya kilimo yamejadiliwa.

Vikao vya Bunge la Kitaifa na Seneti viling'oa nanga mwendo wa saa nane unusu ilivyo desturi siku ya Jumanne huku jukumu la kwanza la mabunge hayo likiwa kujadili uteuzi wa watakaohudumu katika kamati za shughuli za bunge. Wabunge walioteuliwa kuhudumu katika nyadhifa hizo katika Bunge la Kitaifa ni Amos Kimunya wa Kipipiri, Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Turkana, Joyce Emanikor, Shadrack John Mose wa Kitutu Masaba na Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Meru, Kawira Mwangaza.

Wengine ni Mbunge wa Kitui ya Kati, Makali Mulu, Mishi Mboko wa Likoni na Mbunge Maalum, Godfrey Osotsi. Walioteuliwa kuhudumu katika Kamati ya Shughuli za Bunge ya Seneti ni Fatuma Dullo, Cleophas Malalah, Beatrice Kwamboka, Paul Githiomi Mwangi Mohamed M. Mahamud na Christopher, Andrew Langat na Ledama Ole Kina.

Akitoa hoja zake kuhusu uteuzi huo, Seneta Maalum, Isaack Mwaura ameihimiza kamati hiyo kuhakikisha muda unaotengwa kujadili miswada mbalimbali unazingatiwa ili kuepusha hali ya kupoteza muda mwingi katika kujadili suala moja.


Aidha, suala la mgomo wa wauguzi na masaibu ya wakulima wa mahindi katika siku za hivi karibuni ni miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa huku maseneta mbalimbali wakiwamo Moses Wetangula wa Bungoma na Margaret Kamar wa Uasin Gishu wakiyazungumzia na kusema ni jukumu la bunge kuhakikisha masaibu yanayoshuhudiwa katika sekta hizo yanashughulikiwa.

Seneta wa Siaya, James Orengo aidha amezungumzia mapendekezo ya kuifanyia katiba marekebisho huku akiwaomba maseneta kutohofu kufanikisha marekebisho yoyote kwani ni haki ya kikatiba.

Miongoni mwa mapendekezo kuhusu marekebisho ya katiba ni kubuni wadhifa wa Waziri Mkuu na manaibu wake wawili ili kuwapa nafasi ya uongozi wanaoishindwa wakati wa uchaguzi. Hata hivyo pendekezo hilo linapingwa na viongozi mbalimbali akiwamo Naibu wa Rais William Ruto anayesema cha muhimu ni kwa anayeshindwa na kuwa wa pili katika kinyang'anyiro cha urais kupewa wadhifa wa Kiongozi Rasmi wa Upinzani Bungeni.

Masuala mengine makuu yanayotarajiwa kujadiliwa na mabunge hayo baada ya kerejelea vikao ni marekebisho katika Tume ya Uchaguzi, IEBC, bajeti, vilevile mgao wa fedha za kaunti huku Seneta wa Makueni, Mutula Kilonzo Juniour akipinga mipango ya kupunguza bajeti ya kaunti ili kudhibiti gharama za serikali akisema cha muhimu ni kuziwajibisha moja kwa moja kaunti zinazofuja fedha.

Seneta Wetangula ametoa wito wa kukomeshwa kwa siasa za ubabe kati ya Seneti na Bunge la Kitaifa na kuzingatia huduma kwa wananchi. Kesho vikao vya bunge vitaendelea kuanzia saa tatu asubuhi vilevilile awamu ya alasiri kuanzia saa nane unusu huku

Related Topics

Bunge seneti