Ruto asema kampuni ambazo haziweki wazi rekodi za kandarasi zitawajibishwa

Naibu wa Rais, William Ruto amemwagiza Waziri wa Fedha, Henry Rotich kuhakikisha majina ya idara zote za serikali ambazo hazijatimiza agizo la Rais Uhuru Kenyatta la kuweka wazi taarifa kuhusu kandarasi zinazotolewa na idara hizo, yanawasilishwa kwa Mkuu wa Utumishi wa Umma kwa kipindi cha siku thelathini zijazo.

Akihutubu wakati wa kongamano la kufanikisha mipango mbalimbali ya serikali linaloendelea jijini Nairobi, Ruto amesema agizo hilo lilitolewa kufuatia lengo la serikali kudumisha uwazi kuhusu namna inavyotekeleza miradi yake na ni sharti liheshimiwe.

Ruto aidha amesema kuwekwa wazi kwa kandarasi na miradi mbalimbali inayoendelezwa na serikali, kutasaidia kukabili ufisadi na kuimarisha huduma kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa kongamano hilo, Waziri wa Fedha, Henry Rotich aidha amesema kwa kipindi cha miaka michache iliyopita, serikali imepiga hatua kubwa hasa katika kuweka wazi makadirio yake ya bajeti ili kuruhusu umma kutoa maoni mbalimbali.

Gavana wa Vihiga, Wilber Otichilo ambaye pia amezungumza katika kongamano hilo aidha ameelezea umuhimu wa kutolewa kwa taarifa za muhimu ili kufanikisha mipango ya Serikali ya Kitaifa vilevile serikali za kaunti.

Ikumbukwe serikali inalenga kufanya sensa ya watu mwezi Agosti mwaka huu ambayo itaendelezwa kidijitali. Lengo la sensa hiyo ni kufanikisha mipango ya serikali katika ugavi wa fedha na kuhakikisha usawa katika usambazaji wa rasilmali.

Related Topics

Ruto