Duale azomewa na vijana huku wafuasi wa Jubilee na CORD wakitofautiana Kitale

Na, Beatrice Maganga
Mivutano yakisiasa imeshuhudiwa wakati wa ziara za Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto maeneo mbalimbali nchini. Kundi la vijana lilimzomea Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Adan Duale aliyekuwa kwenye ziara mjini Garissa na Rais Kenyatta huku wafuasi wa Jubilee na CORD wakitofautiana wakati wa ziara ya Ruto Kitale.
Mjini Garissa wakazi wanaompinga Duale ambaye pia ni Mbunge wa Garissa mjini walimzomea wakidai kutoridishwa na utendakazi wake. Hata hivyo Rais Kenyatta aliwarai vijana kuwajibika na kusajiliwa kuwa wapigakura ili wapate fursa ya kuwachagua viongozi wanaotaka.Duale kwa upande wake alielezea imani kwamba muungano wa Jubilee utapata ushindi mkubwa wakati wa uchaguzi mkuu ujao.

Mjini Kitale, wafuasi wa Chama cha Jubilee na ODM wamekabiliana vikali wakati wa mkutano wa Naibu wa Rais Wiliam Ruto. Mambo yalianza kwenda kombo pale kila upande wa wafuasi wa vyama hivyo walipoanza kupaaza sauti wakiipigia  debe mirengo yao huku wafuasi wa ODM wakidai kuwa Trans-Nzoia ni ngome ya upinzani.Ilimlazimu Ruto  kuingilia kati kutuliza hali na kuwarai wafuasi wa Jubilee kusajiliwa kuwa wapigakura.
Ikumbukwe siku ya Jumatatu, kundi la vijana liliuzuia msafara wa Ruto kuingia mjini Bungoma hatua iliyomlazimu kutumia barabara tofauti.

 

Related Topics