''Tutatoa msimamo wetu kuhusu waziri wa ugatuzi'' Lasema baraza la mashirika yasiyo ya serikali

Na Carren Omae

Baraza la Mungano wa Mashirika yasiyo ya Serikali mapema leo linatarajiwa kutoa taarifa kuhusu madai kwamba baadhi ya mashirika yalimhusisha Waziri wa Ugatuzi na Mipango ya Kitaifa Mwangi Kiunjuri katika sakata ya ufisadi. Mwenyekiti wa Mashirika hayo Stephene Cheboi amesema watatoa msimamo  kuhusu Waziri huyo.
Siku ya Jumatano Waziri Kiunjuri aliibandua Bodi ya Mashirika Yasiyo ya Serikali ikiwa siku moja tu baada ya bodi hiyo kumtuhumu kuwa aliitisha hongo baadhi ya mashirika hayo.
Hata hivyo mashirika hayo tayari yamejitenga na hati-kiapo iliyowasilishwa kwa Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi, EACC ikimtuhumu Kiunjuri kwa kudai hongo ya shilingi milioni 20.
Katika hati-kiapo hiyo iliyosainiwa na mwanamke kwa jina Delphine Christopher, Kiunjuri kupitia msaidizi wake, Wambui Kimathi alipokea shilingi milioni 10 tarehe 2 mwezi Septemba huku shilingi milioni 10 zaidi zikitarajiwa kulipwa baadaye.
Kiunjuri vile vile alimwachisha kazi kwa muda Mkurugenzi Mkuu wa bodi hiyo, Fazul Mohammed akisema hana tajriba ya kuhudumu katika wadhfa huo.