Maafisa watakaosimamia mitihani kuwajibishwa iwapo wizi utaripotiwa

Na Carren Omae

Maafisa wote wa umma watakaotwikwa jukumu la kusimamia mitihani ya kitaifa ya mwaka huu, watawajibishwa iwapo visa vya udanganyifu katika mitihani hiyo vitaripotiwa. Akizungumza wakati wa kupokea ripoti kuhusu mkataba wa makubalinao kuhusu nyongeza ya mishahara, kati ya Tume ya Huduma za Walimu TSC na Chama cha Walimu KNUT na kile cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kadri KUPPET Rais Uhuru Kenyatta, amesema idara zote zinafaa kuhakikisha visa hivyo havishuhudiwi tena mwaka huu.
Kulingana na Rais mikakati kabambe imewekwa kukabili tatizo hilo.
Tangazo hilo la Rais linajiri siku moja tu baada ya Wizara ya elimu kutoa sheria kali zitakazotumiwa kukabili udanganyifu katika mtihani hiyo. Kulingana na Waziri wa Elimu Fred Matiang'i walimu watakaoisimamia mitihani hiyo hawataruhusiwa kuwa na simu za rununu katika vyumba vya mitihani.
Baraza la Mitihani Nchini KNEC aidha limetangaza kupiga marufuku utumiaji wa bweta yaani geometrical sets huku vifaa ambavyo huwa ndani mfano protactors na dividers vikibebwa ndani ya mfuko unaoonekana hadi ndani.
Ikumbukwe watahiniwa takriban alfu tano walikosa matokeo yao ya mtihani wa KCSE mwaka uliopita kufuatia udanganyifu.