Bernadette Musundi ndiye mwenyekiti wa jopo litakaloshughulikia uteuzi wa makamishna wapya wa IEBC

Na  Carren Omae

Mwakilishi wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki, Bernadette Musundi ndiye Mwenyekiti wa jopo la kuwateua Makamishna wa Tume ya Uchaguzi, IEBC. Musundi ameteuliwa mapema Alhamisi wakati wa kikao cha kwanza cha jopo hilo huku Professa Abdulghafur El-Busaid akiteuliwa kuwa Naibu mwenyekiti.

Akizungumza baada ya uteuzi wake, Musindi ameahidi wakenya kuwa watafanya kila jitihada kuhakikisha makamishna watakaoteuliwa wana uwezo wa kusimamia uchaguzi mkuu ujao bila matatizo yoyote kushuhudiwa.

Anasema wataweka mikakati kuhakikisha watu kumi na moja watakaopendekeza kwa rais uhuru kenyatta watakubalika na wakenya.

Musindi aidha amesema watatekeleza majukumu yao kwa uwazi na kuhusisha washikadau wote. Hata hivyo anasisitiza watazingatia katiba na utaratibu uliosababisha kubuniwa kwa jopo hilo katika kutekeleza wajibu wao.

Jopo hilo linatarajiwa kutangaza kuwa wazi nafasi katika Tume ya IEBC wiki ijayo.

Baada ya mahojiano hayo jopo hilo litawasilisha kwa Rais Uhuru Kenyatta majina ya watu wawili waliohitimu katika nafasi ya mwenyekiti na wengine tisa katika nyadhfa za makamishna. Kisha Rais atamteua mmoja katika wadhfa wa mwenyekiti na sita kuwa makamishna. Katika kipindi cha siku saba baada ya kupokea majina hayo, Rais atatakiwa kuiwasilisha orodha ya aliowateua kwa Bunge la Kitaifa ili yaidhinishwe kwa mujibu ya sheria za uteuzi wa maafisa wa umma. Bunge litakapoidhinisha majina hayo, Rais Kenyatta aidha atawateua rasmi Makamishna wa tume hiyo kwa kuchapisha majina yao katika gazeti rasmi la serikali.
Jopo hilo litavunjwa baada ya uteuzi huo kukamilika.