Hatma ya Kinisu i mikononi mwa wabunge

Na, Sophia Chinyezi

Hatma ya Mwenyekiti wa Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi EACC, Philip Kinisu itaamuliwa na Bunge la Taifa baada ya Kamati ya Haki na Masuala ya Sheria kuwasilisha bungeni ripoti inayopendekeza kubanduliwa kwake. Kamati hiyo iliyo chini ya uwenyekiti wa Mbunge wa Ainabkoi, Samuel Chepkonga imesema hoja zilizowasilishwa dhidi ya Kinisu zina uzito.
Iwapo wabunge wataiidhinisha ripoti hiyo, Rais Uhuru Kenyatta atahitajika kubuni jopo la kumchunguza Kinisu na huenda akalazimika kuondoka ofisini. Kinisu amekuwa akikabiliwa na shinikizo la kujiujulu baada ya kubainika kuwa kampuni yake kwa jina Esaki, ililipwa fedha nyingi na Taasisi ya Taifa ya Huduma za Vijana NYS kupitia miradi iliyochangia kufujwa kwa kima cha shilingi milioni 791 za taasisi hiyo.
Albert Mokono Ondieki ambaye aliwasilisha hoja hiyo, alikuwa ameitaka Kamati ya Haki na Masuala ya Sheria kutathmini madai dhidi ya Kinisu kisha kubuniwa kwa jopo la kumchunguza.