Bunge la kitaifa lakosa kupitisha ripoti kuhusu IEBC huku Seneti ikiidhinisha

Na, Carren Omae

Bunge la Kitaifa limeahirisha mjadala wa ripoti ya kamati ya bunge ya pamoja kuhusu mabadiliko katika Tume ya Uchaguzi IEBC na mfumo wa uchaguzi nchini. Wabunge wamekosa kuafikiana kuhusu iwapo ripoti hiyo inafaa kupitishwa jinsi ilivyo au ifanyiwe marekebisho kwanza, jambo lililomlazimu Naibu Spika, Joyce Laboso kuahirisha vikao.
Wabunge wengi wamependekeza ripoti hiyo kufanyiwa marekebisho hasa katika kipengele kinachowapiga marufuku wanasiasa kuvihama vyama vyao baada ya uteuzi wa wawaniaji wa nyadhifa mbalimbali kukamilika. Ababu Namwamba ni Mbunge wa Budalang'i.
Hata hivyo Kiongozi wa Wengi, Adan Duale amepinga utaratibu uliotumika kuidhinisha marekebisho kwenye ripoti hiyo.
Awali wabunge walipinga hoja ya kuahirisha vikao vya kujadili ripoti hiyo. Hoja ya kuahirishwa kwa vikao hivyo iliwasilishwa na Mbunge wa Ainamoi Benjamin Langat. Jumla ya wabunge 20 waliunga mkono hoja hiyo huku 92 wakiipinga hivyo kuruhusu mjadala kuendelea.
Seneti kwa upande wake imeidhinisha ripoti hiyo bila kushuhudiwa kwa mjadala mkali, huku wengi wakisema inafaa. Hata hivyo baadhi ya maseneta wameipinga hasa kuhusu pendekezo la kuwazuia wanasiasa kuvihama vyama vyao baada ya vyama hivyo kukamilisha uteuzi wa wanaowania nyadhifa mbalimbali. Wlfred Machage ni Seneta wa Migori.