Ruto asisitiza vita dhidi ya ufisadi vinawalenga baadhi ya watu

Naibu wa Rais William Ruto ameendeleza shtuma dhidi ya baadhi ya watu anaodai kuwa wanatumia vita dhidi ya ufisadi kuisambaratisha miradi ya serikali ya Jubilee. Akizungumza kwenye kaunti ya Mandera wakati alipoongoza shughuli ya utoaji wa chakula cha msaada, Ruto amesema kuwa kwa miaka michache ambayo Jubilee imekuwa madarakani imezipiku zile zilizotanguliwa kupitia rekodi ya maendeleo. Amewataka wanaoishtumu mara kwa mara kukoma kwani wanachochea wananchi wasio na ufahamu wowote kuhusu nia yao potovu.
 
Akionekana kumlenga Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga, Ruto amedai kuwa anaendesha siasa za ukabila huku akijidai kuwa anawaunganisha Wakenya.
 
Amesisitiza watakaoamua ni nani kiongozi wa taifa hili, ni Wakenya kupitia uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.
 
Hayo yakijiri wabunge wa Chama cha Jubilee wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi katika bunge la Kitaifa Adan Duale wametoa wito kwa Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto kukilinda chama, wakidai kuna maadui wanaotaka kukisambaratisha.
 
 
 

Related Topics

ruto Ufisadi