Ni vyema kudhibiti kiwango cha pesa zinazotumika wakati wa kampeni

Naliunga mkono pendekezo la Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) linalohusu udhibiti wa ufadhili wa uchaguzi na pia kampeni kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Mapendekezo hayo yanayolazimu vyama vya kisiasa na  watakaogombea viti mbalimbali kuunda kamati za kusimamia fedha za kuendesha kampeni zao,mipaka iliyotolewa kuhusiana na ufadhili wa watu binafsi na mashirika kwa wawaniaji, yatasaidia Wakenya kuwachagua viongozi kulingana na rekodi yao ya utendakazi pasi na kuzingatia ukwasi na ubabe wao kifedha.

Mswada huo umekuja wakati ambapo wanasiasa wanafuja mali ya umma ili kuitumia kufadhili kampeni zao. Ni pendekezo ambalo lafaa kuigwa ili kudhibiti mabilioni ya pesa inayotumika wakati wa uchaguzi kama ilivyoshuhudiwa katika uchaguzi uliopita.

Yafaa mapendekezo hayo yaidhinishwe na Bunge ili kuinusuru fedha za wananchi zinazotumiwa visivyo. Mabwanyenye wanaowafadhili wanasiasa kwa lengo la kupewa kandarasi pia watadhibitiwa ili ufadhili wao usipite kiwango fulani.

Kuna msukumo na dhana potovu miongoni mwa wanasiasa, hivi kwamba wao hufuja mali ya umma ili kijiimarisha kisiasa. Naamini mswada huu utakuwa kiboko yao, hasa wasiokuwa na rekodi nzuri ya utendakazi.