×
App Icon
The Standard e-Paper
Join Thousands Daily
★★★★ - on Play Store
Download App

Wasanii wa Little Theatre Mombasa wahakikishiwa kutofurushwa na serikali

 

Katibu wa Wizara ya Uchukuzi, Mohammed Daghar akihutubia wana habari. [Robert Menza, Standard]

Katibu wa Wizara ya Uchukuzi, Mohammed Daghar, amewahakikishia wasanii wanaotumia ukumbi wa Little Theatre uliopo katika Kaunti ya Mombasa kuwa hawatafurushwa kutoka katika ardhi hiyo, licha ya mipango ya Shirika la Reli nchini (Kenya Railways Corporation) kuanzisha mradi mpya wa ujenzi wa chuo cha mafunzo ya reli.

Daghar ametoa hakikisho hilo baada ya kikao kilichowakutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli nchini, Philip Mainga, pamoja na viongozi wa wasanii kutoka Kaunti ya Mombasa.


Kikao hicho kimelenga kutafuta mwafaka kuhusu mustakabali wa ukumbi wa Little Theatre, ambao kwa miaka mingi umekuwa kitovu cha shughuli za sanaa na burudani katika eneo la Pwani.

Kwa mujibu wa Daghar, serikali inatambua mchango mkubwa wa wasanii katika kukuza utamaduni, kutoa ajira kwa vijana na kuimarisha sekta ya ubunifu.

Amesisitiza kuwa serikali haina nia ya kuwaathiri wasanii wala kuvunja shughuli zao bila kuwahusisha kikamilifu katika maamuzi yanayowahusu.

“Tumekubaliana kuwa kutaundwa kamati itakayojumuisha wawakilishi wa Wizara ya Uchukuzi, Shirika la Reli nchini, serikali ya Kaunti ya Mombasa pamoja na viongozi wa wasanii.

Kamati hiyo itakuwa na jukumu la kufanya mashauriano ya kina na kutoa mapendekezo yatakayohakikisha maslahi ya pande zote yanazingatiwa,” amesema Daghar.

Aidha, Daghar ameeleza kuwa kamati hiyo itapewa muda wa mwezi mmoja kukamilisha kazi yake na kuwasilisha ripoti itakayobainisha njia bora ya utekelezaji wa mradi wa chuo cha mafunzo ya reli bila kuathiri shughuli za sanaa katika ukumbi wa Little Theatre.

Viongozi wa wasanii waliokuwepo katika kikao hicho wamepongeza hatua ya serikali kuwasikiliza na kuwahakikishia usalama wa shughuli zao.

Wameeleza matumaini kuwa kamati itakayoundwa itazingatia umuhimu wa ukumbi wa Little Theatre kama urithi wa kitamaduni na kituo muhimu cha kukuza sanaa katika Kaunti ya Mombasa.

Kwa sasa, wasanii wamehimizwa kuendelea na shughuli zao kama kawaida huku wakisubiri mapendekezo ya kamati hiyo, huku serikali ikiahidi kuwa hakuna hatua yoyote ya kuwaondoa itakayochukuliwa kabla ya mashauriano kukamilika.