×
App Icon
The Standard e-Paper
Informed Minds Prefer The Standard
★★★★ - on Play Store
Download Now

Matokeo ya chaguzi ndogo, mtihani wa 2027

Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula akipiga kura yake katika kituo cha Namakhele Primary School, wadi ya Chewele–Kabuchai, Novemba 27, 2025. [Benjamin Sakwa, Standard]

Kugombea kiti katika uchaguzi huleta shinikizo lisilo la kawaida, hata wanasiasa waliokomaa hujikuta wakitetereka.

Lakini katika chaguzi ndogo za leo, uzito mkubwa haupo tu kwa wanaogombea, bali kwa ‘magodfather’ wa siasa ambao hawapo kwenye debe, lakini ndio wanaoweka kila kitu rehani.

Huu ndio mtihani wao wa mapema kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Katika maeneo mbalimbali, vigogo wa kisiasa wanatumia chaguzi hizi kama kipimo cha ushawishi wao. Wamewekeza fedha, rasilimali, muda na mawakala, wakifahamu vyema kwamba kushindwa kwa wagombea wao kutafunua udhaifu wao hadharani na kuharibu hadhi yao ya kisiasa.


Kwa upande wa UDA yake Rais William Ruto na ODM, chaguzi hizi ni zaidi ya ushindani wa vyama; ni majaribio ya mapema ya nguvu, mikakati na nafasi za uongozi ndani ya kambi zao. Katika hali hii, wagombea wamegeuka chambo katika mchezo mpana unaoendeshwa na walengwa wa madaraka wanaotaka kujijenga au kuwadhoofisha wenzao kabla ya mwaka wa 2027.

Katika eneo la Magharibi mwa nchi,  Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula wanajaribu kuthibitisha uwezo wao wa kuunganisha eneo hilo nyuma ya Rais Ruto. Hata hivyo, kampeni za Malava na Chwele zimeweka wazi changamoto wanazokabiliana nazo, huku Gavana George Natembeya akijitokeza kama mshindani mpya anayevuruga hesabu zao. Wakati uo huo, Rais Ruto amewekeza pakubwa katika eneo hili, akilenga kuziba pengo lililoachwa na Raila Odinga baada ya kupungua kwa ushawishi wake wa miaka mingi.

Kaskazini mwa Mlima Kenya, Mbeere Kaskazini imegeuka uwanja wa mapambano kati ya Rais Ruto, kupitia Kithure Kindiki na aliyekuwa Naibu wake Rigathi Gachagua. Kinyang’anyiro hiki kimegeuka jaribio la wazi la kuonyesha ni nani mwenye usemi mzito zaidi katika siasa za mlimani. Kwa Kindiki, mambo ni mazito zaidi kwani ushindi unamweka mstari wa mbele wa kuwa mgombea mwenza wa Ruto mwaka 2027, ilhali kushindwa kunaweza kumvunja nguvu katika mbio hizo.

Katika eneo la Nyanza, eneobunge la Kasipul limefufua mpasuko wa zamani ndani ya ODM. Gavana Gladys Wanga na Waziri John Mbadi, wanaotajwa kama warithi watarajiwa wa Raila Odinga, wanamuunga mkono kijana Boyd Were wa ODM, lakini pia wanatumia uwanja huu kupimana uzito. Hata hivyo, naibu wa Wanga, Oyugi Magwanga, amevunja safu kwa kumuunga mkono mgombea huru Philip Aroko, anayeongezewa nguvu na Okoth Obado.

Eneo la Pwani, kiti cha Magarini, kilichorudiwa baada ya ushindi wa Harrison Kombe kubatilishwa, kimewavutia tena vigogo. Stanley Kenga wa DCP anapata msukumo mpya baada ya Samuel Nzai kujitoa na kumuunga mkono, huku Hassan Joho, Amason Kingi na Gideon Mung’aro wakiongoza juhudi za kuiwezesha ODM kurejesha kiti hicho.

Katika kaunti ya Kisii, aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i ameweka nguvu zake katika kupinga juhudi za UDA kuchukua viti vitatu vya wadi.

Na kama ilivyo katika siasa za Kenya, matokeo ya kesho hayataashiria tu washindi na walioshindwa, bali yatatoa fununu ya wazi kuhusu nani kati ya vigogo wa leo atasimama imara, na nani atateleza kimyakimya kabla ya safari ya 2027 kuanza rasmi.