Na, Rosa Agutu
Vijana wengi nchini pamoja na raia wenye mapato ya chini wamekuwa wakikandamizwa kisheria pindi wanapotuhumiwa kwa makosa mbalimbali. Hayo yamebainishwa katika ripoti iliyoandaliwa na Baraza la Kitaifa kuhusu Haki na kuzinduliwa rasmi na Jaji Mkuu, David Maraga. Kulingana na ripoti hiyo, asilimia 75 ya wanaozuliwa kwenye korokoro za polisi ni vijana wenye kati ya umri wa miaka 18-35. Imebainika kwamba vijana wengi hutiwa mbaroni wakiwa katika harakati za kuendeleza uchuuzi wa kujifatutia riziki bila leseni.
Wengine pia hukamatwa wakiwa katika maeneo ya burudani. Kulingana na Maraga, huo umebainisha kuwa asilimia 63 ya washukiwa wa makosa mblimbali huachiliwa huru bila kuwepo kwa rekodi rasmi kuhusu sababu za kuachiliwa kwao.
Aidha, ripoti hiyo inaonyesha kwamba asilimia 49 ya visa vya mauaji vimetekelezwa na wanawake ikilinganishwa na asilimia 32 ya wanaume. Vilevile kesi nyingi za wizi wa bidhaa zimewahusishwa wanawake walioajiriwa kuwa vijakazi wa nyumbani.
Licha ya ripoti hiyo kubainisha kwamba visa vya unajisi wa watoto vimeongezeka, ni asilimia tano pekee ya visa hivyo ambapo wahusika huhukumiwa huku asilimia 60 ya kesi hizo zikiondlewa mahakamani.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mwanasheria Mkuu wa serikali, Prof Githu Muigai amesema ripoti hiyo itasaidia kukabili visa vya ubaguzi na kuhakikisha wananchi wanatendewa haki. Na huku shughuli ya kuwasajili wapigakura wapya ikiendelea, Muigai ametoa wito kwa Tume ya Uchaguzi, IEBC kufanikisha usajili wa wafungwa.