Kinyume na ilivyotarajiwa, Rais Uhuru Kenyatta amekwepa kuzungumzia suala lililochochea hisia kali la maafisa wa polisi kupungiziwa mishahara, badala yake kulenga masuala mengine yanayohusu usalama wa nchi. Akizungumza alipoongoza hafla ya kufuzu kwa makurutu katika Chuo cha Mafunzo cha Kiganjo, Rais amesema mpango wa kushirikiana miongoni mwa taasisi mbalimbali wakati wa kukabili visa vya utovu wa usalama nchini, umechangia pakubwa kukabiliwa kwa tishio hilo. Amezitaja hatua zilizopigwa kuwakabili magaidi kuwa mojawapo ya mafanikio hayo. Rais amesema ana imani kuwa waliofuzu leo wataendeleza mpango huo wa serikali.
Rais aidha amewashauri kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kuzingatia waliofunzwa chuoni humo katika utendakazi wao. Rais amewashauri kudumisha uhusiano mwema na raia wa maeneo watakayotumwa kuhudumu ili kuboresha sifa za idara hiyo.