Nchi 31 ambako hakuzikwi waliofariki

Wafanyikazi wa kaunti ya Nairobi wakitayarisha sehemu ya kuchoma maiti katika makaburi ya Lang'ata.

Mdahalo umezuka tangu kuteketezwa kwa mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Safaricom, Robert “Bob” Collymore na wakenya wengine mashuhuri hivi karibuni kuwa sababu yake halisi ya kupitia mfumo huo ni nini haswa.

Wakenya hao mashuhuri ambao miili yao ilipitia mfumo huo ni pamoja na aliyekuwa mwanaharakati wa uhifadhi wa Mazingira Bi. Wangari Maathai aliyefariki mwaka 2011, aliyekuwa kiongozi wa upinzani Keneth Matiba, aliiyekuwa mchezaji golf maarufu Peter Njiru, aliyekuwa waziri Peter Okondo, Askofu wa Kanisa la Kianglikana Manasses Kuria na mkewe Nyambura Kuria.

Mwaka uliopita John Macharia mwana wa mkurugenzi wa Royal Media S.K Macharia aliyefariki mwaka uliopita baada ya kuhusika katika ajali ya barabarani mwili wake pia ulitekeketwa badala ya mazishi ya kawaida.

 Jambo la kustaajabisha ni kwamba katika shughuli za watu hao wote sherehe za kuteketeza miili zimehudhuriwa tu na familia na watu wa karibu.

Historia ya uteketezaji maiti

Kuteketeza maiti kama sehemu ya mfumo wa mazishi kumefanyika tangu jadi zaidi ya miaka 10,000 iliyopita. Nchini China miili imekuwa ikiteketeza kuanzia miaka 8000BC yaani kabla kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

Huko Ugiriki, uteketezaji maiti umekuwa ukifanyika tangu mwaka 480BC na nchini Sweeden desturi hiyo imekuwepo tangu jadi na kukomesha yapata miaka 1,000 iliyopita baada ya dini ya Ukristo kuingia huko. Baada ya injili ya Kristo kuenezwa barani Ulaya, desturi hiyo ilififia kwani Wakristo waliitaja kuwa kinyume na maadili ya dini.

Hadi miaka ya 1900, Kanisa Katoliki lilijitokeza na kupinga desturi hiyo. Mfumo wa kisasa wa kuteketeza maiti ulianza miaka ya 1800 baada ya kuvumbuliwa kwa tanuri ya kisasa na moto na Professor Brunetti, aliyeiwasilisha katika maonyesho makubwa ya Elimu na Utamaduni mjini Vianna, Austria mwaka 1873.

 Leo hii uteketezaji wa maiti unafanyika katika maataifa 31 ulimwenguni ambapo zaidi ya asilimia 75 ya wafu nchini Uswizi huteketezwa Dini ambazo zimekubali desturi hiyo ni Hindu, Jain na Sikh huku Wakristo na Waislam wakiipinga.

Kufikia miaka ya 1960, dini ya Kikristo ililegeza msimamo na kukubali desturi ya kuteketeza wafu ila kwa ruhusa kutoka kwa askofu. Kufariki kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Safaricom Robert “Bob” Collimore na hatimaye kuteketezwa katika makaburiya Kariakor mjini Nairobi siku moja baadaye kumezua mjadala mkubwa wa iwapo kweli tunahitaji kuingia gharama ya mamia ya maelfu ya pesa kuzika wafu.

Bob Collymore aliyefariki Jumatatu tarehe mosi mwezi huu wa Julai mwili wake haukuzikwa bali uliteketezwa siku iliyofuata kwenye sherehe iliyohudhuriwa na watu wachache ikiwemo familia na marafiki.

Uteketezaji wa miili nchini Kenya na ulimwenguni umekuwa si jambo geni tena na umekuwa mfumo maarufu kwa baadhi ya watu mashuhuri kuwaweka wapendwa wao walioaga dunia mapumzikoni.

Uteketezaji wa miili hufanywa katika eneo la makaburi ambako kuna sehemu maalum iliyo na tanuri ya moto mkali unaoteketeza mwili wa marehemu na kusalia jivu lisilozidi nusu kilo. Jivu hilo baadaye huwekwa katika kasha dogo na kukabidhiwa familia ili waende wahifadhi kama kumbukumbu.

Katika kuuteketeza mwili wa marehemu, idhini ni sharti iwe imetoka kwa wasia wa marehemu mwenyewe au mtu wake wa karibu aliyemteua yaani “next of kin” na vilevile kutoka kwa taasisi ya afya ya serikali.

Stakabadhi zinapokubaliwa na kutiwa saini mwili huruhusiwa kupelekwa katika eneo la uteketezaji kwa shughuli kuanza.

Desturi ya kuteketeza maiti ni maarufu katika jamii ya Wahindi ingawaje katika sehemu nyingine za ulimwengu hasa Ulaya na Marekeni desturi hiyo inaendelezwa kutokana na gharama ya chini.

Kenya ina takriban vituo 18 vya tanuri za uteketezaji maiti. Kati ya hivyo, vile vinavyofahamika zaidi mjini Nairobi ni kile cha makaburi ya Langata na makaburi ya Kariokor huku vituo vingine vikiwa vya Wahindi, Hindu Crematorium vilivyoko katika miji Mikuu ya Nairobi, Mombasa, Kisumu na miji mingine iliyo na idadi kuba aya jamii ya Wahindi.

Gharama ya uteketezaji maiti

Gharama ya kuteketeza maiti inaanzia Kshs.10,000 hadi Kshs.100,000 kulingana na ni wapi unafanyia shughuli hiyo. Katika makaburi ya Langata gharama ni Kshs.16,800 kwa mtu mzima na mtoto Kshs.12,000.

Katika vituo vya Hindu Crematorium, gharama ni Kshs. 10,000 kwa mwanachama na Kshs22,000 kwa wasiokuwa wanachama. Ni kutokana na gharama hii ya chini ambapo baadhi ya jamii au watu binafsi huamua wasindikizwe kupitia njia hii ili kupunguza gharama ya mazishi ya kawaida.

Inakadiriwa kuwa mazishi ya kawaida hugharimu kati ya shilingi 100,000 na 1,000,000 huku gharama ya kuteketeza mwili ikiwa chini ya shilingi 40,000.

Mazishi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Safaricom, marehemu Bob Collymore yaligharimu shilingi 37,500 pekee zikiwemo shilingi 15,000 za kusafirisha mwili huo na shilingi 22,800 za kuuteketeza.

Aliwacha wasia

Bob Collymore ambaye alifariki baada ya kuugua maradhi ya saratani ya damu aliamua yeye mwenyewe kwamba mwili wake usizikwe kaburini bali uteketeWzwe.

Marehemu ambaye ni raia ya Uingereza hakutaka mwili wake usafirishwe hadi Uingereza kuzikwa kutokana na gharama ya juu ya mazishi nchini mwake.

Katika mitandao ya kijamii, kuteketezwa kwa mwili wa Bob Collymore kumezua mdahalo wa iwapo kweli Wakenya wanahitaji kuchangisha mamia ya maelfu ya pesa kwa ajili ya mazishi.

Baada au kabla mwili kuteketezwa jamii inaweza kufanya sherehe fupi ya matanga ambayo gharama yake ni ya chini vilevile. Uteketezaji wa maiti huipa jamii afueni ya kupumua kifedha na kiakili na hivyo desturi hiyo inazidi kuwa maarufu duniani.

Kunao wale wanaounganisha utetekezaji na matanga ya kiasili ambapo baada ya mwili kuteketezwa wanachukua kasha la majivu na kuenda nalo nyumbani kwa sherehe za matanga.