×
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The Standard Group is recognized as a leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national and international interest.
  • Standard Group Plc HQ Office,
  • The Standard Group Center,Mombasa Road.
  • P.O Box 30080-00100,Nairobi, Kenya.
  • Telephone number: 0203222111, 0719012111
  • Email: [email protected]
Premium

Wanasayansi watafuta njia za kutengeneza chakula cha Flamingo

News

Ziwa Nakuru ni maarufu kwa maelfu ya ndege aina ya flamingo, na ndicho kivutio kikubwa cha watalii nchini Kenya lakini katika miaka ya hivi karibuni, kupungua kwa idadi ya ndege hao kumeshuhudiwa, ambapo wataalamu wanasema hali hii imesababishwa na ongezeko la maji ziwani humo na kuchangia ukosefu wa chakula. Kwa sasa wanasayansi wameanzisha mchakato wa kutafuta chakula mbadala kuwasaidia ndege hao aina ya flamingo.

Katika ziara ya Radio Maisha katika mbuga ya wanyama ya Ziwa Nakuru katika halfa ya Wanahabari iliyoandaliwa na Taasisi Inayoshughulikia masula ya mazingira Sayansi Afya na Kilimo yaani Media for Environment, Science, Health and Agriculture in Kenya (MESHA) tulipata maelfu ya ndege hawa aina ya flamingo wakielea na kutambaa juu ya ziwa, wakipaka ukingo wa Kusini mwa Ziwa rangi ya waridi. Ziwa Nakuru limeorodheshwa kuwa mojawapo la maziwa yenye kupendeza zaidi duniani, na kivutio chake maarufu kikiwa ni ndege hawa aina ya flamingo.

Kuongezeka kwa kiwango cha maji katika ziwa hili kwa takriban miaka kumi sasa kumeathiri flamingo. Tatizo sawa na hili linashuhudiwa katika maziwa mengine ya chumvi-chumvi yakiwamo Bogoria, Elementaita, Solai, Simbi Nyaima na Natron.

"Ongezeko la kiasi cha maji safi huathiri kemia ya ziwa. Hapo awali, viwango vya pH vya Ziwa Nakuru vilifikia 10.5, na hivyo kujenga mazingira bora ya uzalishaji wa chakula cha flamingo. Kuongezeka kwa viwango vya maji hata hivyo kumesababisha viwango vya pH kupungua hadi 9.5," Mtafiti Mkuu wa Huduma ya Wanyamapori nchini Kenya Joseph Edebe alisema

Kauli yake inasisitizwa na Mkuu wa Hifadhi ya Ziwa Nakuru Edward Karanja ambaye anasema Flamingo kawaida hula mwani unaokua kwa hali ya alkali, kwa hivyo kwa kupungua kwa alkali ya maji tunaona lishe ndogo ya flamingo ambayo ndiyo chanzo cha idadi yao kupungua.

Hata hivyo kulingana na Karanja Idadi ya ndegeg ambao mara kwa mara upatikana katika maji safi wameongezeka .

"Hali ya kuongezeka kwa Maji ziwani imeleta aina mpya za ndege ambao ni wa kawaida katika maziwa ya maji safi. Wakati wa mvua kubwa, aina fulani za samaki walipata njia yao kutoka kwenye mabwawa ya karibu hadi kwenye ziwa, ambako walistawi. Hii ilisababisha idadi ya aina ya ndege wanaokula samaki kuwa jambo la kawaida ndani ya ziwa," mlinzi wa Hifadhi ya Ziwa Nakuru Edward Karanja alisema.

Idadi inayopungua ya ndege hao, wataalam wanasema, inahusishwa moja kwa moja na viwango vya maji vinavyoongezeka ambavyo vimesababisha kupungua kwa chakula chao.

Takwimu kutoka kwa hesabu za ndege wa majini zilifichua mwelekeo wa kupungua kwa idadi ya ndege hawa ndani ya Ziwa Nakuru ambao wakati fulani walijulikana kwa kuhifadhi maelfu ya flamingo. Mnamo Januari 2021, takwimu zilionyesha kuwa kulikuwa na flamingo 6,000 katika Ziwa Nakuru ikilinganishwa na mwaka wa 2000 wakati kulikuwa na flamingo 850,000 .

Na sasa wanasayansi wanachunguza njia za kusaidia kutengeneza chakula cha flamingo ili kutatua changamoto hizo.

DaktariJudith Nyunja, ni mwanasayansi mkuu katika Taasisi ya Utafiti na Mafunzo ya Wanyamapori ya Kenya.

"Tunatafuta njia ambazo tunaweza kuongeza uzalishaji wa chakula kwa kutumia sayansi. Changamoto kubwa inayowakabili flamingo kwa sasa, hasa flamingo wadogo ni ukosefu wa chakula cha kutosha. Mradi huo unaojulikana kama mradi wa Spirulina unatarajiwa kutatua hili," Daktari Nyunja .

Kulingana na Nyunja mradi huu uko katika hatua za mwanzo mwanzo, na unahusu kueneza mwani wa bluu-kijani yaani blue-green algae katika maabara kabla ya kuwekwa kwenye mazingira asilia ambapo unatarajiwa kustawi.

"Tunataka kueneza Spirulina katika mipangilio ya maabara kisha kuipeleka kwenye mabwawa ambapo tutafuatilia mara kwa mara ambayo flamingo wanatembelea kutafuta chakula. Ikifaulu katika mabwawa ya maandamano, tutaitambulisha kwa wingi kwenye maziwa haya," Nyunja aliongeza.

Kuongezeka kwa viwango vya maji hakuathiri tu maeneo ya malisho, bali pia kumeathiri Ziwa Natron la Tanzania, eneo pekee la kawaida la kukua kwa ndege hao katika eneo la Afrika Mashariki.

Takwimu kutoka Shirika la Nature Tanzania, mshirika wa Bird Life International nchini Tanzania kutoka 2018 hadi 2021 zinaonesha kushuka kwa kasi kwa maeneo yao ya kulia katika Ziwa Natron nchini humo.

Katika takwimu kuhusu idadi ya ndege za majini mwaka wa 2018, flamingo walikuwa 760,000, wakiwamo vifaranga 120,000. Kufikia 2019, flamingo milioni 1.7 walihesabiwa pamoja na vifaranga 955,000. Kufikia 2020, ni flamingo 250 tu waliohesabiwa pamoja na vifaranga 35. Mwaka wa 2021, ni 1,900 tu ndio waliohesabiwa. Mwaka uo huo, hakuna viota vilivyorekodiwa.

Mbali na kupanda kwa viwango vya maji, majitaka na taka za plastiki kutoka jiji la Nakuru pia zimeathiriwa pakubwa ziwa hilo.

Ziwa hili lilirekodi hasara inayokadiriwa kuwa zaidi ya shilingi milioni 400 kutokana na miundombinu na vifaa vilivyozama ziwani.

Hata wakati wanasayansi na watafiti wakijaribu kutafuta suluhu ya kupungua kwa idadi ya flamingo, mwezi ujao mataifa mengi yataelekea Misri kwa ajili ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, unaojulikana kama COP27, na Hasara na uharibifu unaosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa ni mojawapo ya vipengele muhimu kwa ujumbe wa Afrika.

"Hasara na uharibifu kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa itakuwa moja ya masuala muhimu Kenya na nchi za Afrika wata wasilisha katika COP 27"Mkurugenzi Mtendaji wa Media for Environment, Science, Health and Agriculture (MESHA) asema

Kauli ya Aghan inasisitizwa na Mkurugenzi wa Power Shift Africa Mohamed Adow. Kulingana naye, mabara ya Afrika yanachangia kwa kiasi kidogo zaidi athari za mabadiliko ya hali ya hewa lakini badala yake yameathirika zaidi kutokana na athari hizo.

"Kwa kiasi kikubwa Afrika inateseka sana kutokana na uzalishaji wa hewa ukaa kutoka kwa nchi tajiri zilizoendelea duniani ambazo zinasababisha mabadiliko ya tabianchi, na hivyo wale ambao wamesababisha mabadiliko ya tabianchi wanapaswa kubeba jukumu kubwa zaidi', Asema Adow.

Related Topics


.

Popular this week

.

Latest Articles