×
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The Standard Group is recognized as a leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national and international interest.
  • Standard Group Plc HQ Office,
  • The Standard Group Center,Mombasa Road.
  • P.O Box 30080-00100,Nairobi, Kenya.
  • Telephone number: 0203222111, 0719012111
  • Email: [email protected]

Jicho Pevu: Duka ya nyama haikosi paka

News
 Leo hii maskini jeuri atakuambia kuwa serikali yao na Uhuru Kenyatta iko imara ilhali maskini huyo huyo hajui cha kula jioni

Kenya ni duka ya nyama, na paka wanaofaidika na nyama hii ni serikali ya Uhuru na Ruto.

Serikali ambayo imesahau majukumu yake ya kulinda na kuhudumia wakenya kwa mujibu wa katiba. Serikali ambayo imejaa wezi ambao kila mara wanapoiba na kisha kubanwa na sheria za taifa basi mahakama yao inakuwa ni kabila zao.

Wezi hawa hukimbilia kabila zao wanaposhikwa na mnofu na kusema eti kabila lao ndilo linalolengwa. Watu wao watakutusi kila unapoibandika serikalijina la ‘mwizi’.

Ajabu ni kwamba wakiiba na kula hawaibi na kabila zao. Leo wanaobaka demokrasia Kenya wako radhi kutoa amri ya wahalifu wa mifugo kupigwa risasi hadharani huku amri ya kuwaangamiza wezi walio uongozini ukinyamaziwa.

Walioiba fedha za NYS hawakupigwa risasi, walioiba fedha za Eurobond hawakupigwa risasi. Walioiba ardhi ya shule ya msingi ya Lang’ata hawakupigwa risasi, walioiba fedha za michezo huko Brazil hawakupigwa risasi.

Leo hebu nijifanye mjinga na kuuliza, ni kwa nini walioiba mifugo wapigwe risasi? Hakika sisi walalahoi ndio wajinga wa kuabudu viongozi hawa wasio na doa ya uongozi. Mwezi mmoja uliopita nilikutana na madereva wa texi mkabala na duka moja la nyama mtaa wa South C.

Niliwaskia kwa umbali wakinitaja na kunijadili huku wakisema kuwa mimi hupenda kupiga vita serikali yao. Niliendelea kuwaskiza kwa mbali kiasi cha kunibidi mimi kupiga kambi hapo na kuingilia mjadala wao.

Kisha mmoja wao aliniuliza kwa nini napenda kupiga vita serikali ya Uhuru Kenyatta? Kwanza nilimtaka afahamu kuwa Uhuru Kenyatta sio serikali. Serikali ni wananchi wakenya. Kabla ya kumaliza sentensi, wa pili aliruka na kusema kuwa hawatakubali mjaluo atawale Kenya.

Kisa na maana, hawatalipa kodi ya nyumba ya jamii ya wakikuyu. Huu ndio ukiritimba wa hali ya juu! Fikra za kikabila na sumu za chuki walizolishwa na makaburu weusi na wabaya zaidi kushinda makaburu weupe kutoka jamii zao.

Kwanza nilibaini kuwa aliyekuwa akipiga domo kuhusu masuala ya Mjaluo kutolipa kodi ya nyumba hana hata kibanda cha kuku. Pili hajawahi kukutana ana kwa ana na Raila Odinga au hata kumkaribia mita mia moja. Nilipomuuliza uhasama wake na jamii ya wajaluo imetoka wapi alifyata domo na kusema kuwa ni mambo waliyotiwa akilini tangu utotoni na vizazi vilivyotangulia.

Katika pita pita zangu kwengineko katika barabara ya Luthuli nilikutana na jamaa mwengine ambaye alisifia kazi yangu na kunipaka marashi. Dakika chache baadaye aligeuka na kuniambia kuwa anaipenda kazi yangu lakini niachane na serikali ya Uhuru Kenyatta.

Hakika dunia tambara mbovu, ukabila umekuwa chakula cha mchana kwa jamii maskini ambayo asilimia kubwa ni sisi. Hakuna mtu mjeuri Kenya kama maskini. Yeye hutumika kutetea wezi, wabakaji, wauaji na wahalifu sugu kwa nembo ya ukabila.

Leo hii maskini jeuri atakuambia kuwa serikali yao na Uhuru Kenyatta iko imara ilhali maskini huyo huyo hajui cha kula jioni. Maskini huyo hana hata kazi. Leo nataka ifahamike wazi kuwa wingu limetanda na dawa ya wahuni wote walio uongozini imekaribia.

Muungano wa wakenya umeanza vuguvugu la tatu. Kenya hii hamna serikali ya Uhuru Kenyatta wala William Ruto. Serikali iliyo madarakani ni serikali ya Wakenya wanaotaka uongozi bora. Iwapo Uhuru na Ruto wameshindwa, na najua wameshindwa waanze kuhesabu siku zao uongozini maana siku ya kuzalishwa ni tarehe nane Agosti mwaka huu.

Wawili hawa wamefanya taifa hili kuwa taifa la kilio kila kukicha. Watu kadhaa wameuawa huko Baringo na maeneo ya Pokot, baa la njaa linawamaliza wakenya, ujinga, ukiritimba, elimu tasa, ukosaji wa ajira, ufisadi, mauaji ya wakenya, uuzaji wa mali na ardhi ya serikali inazidi kuyumbisha taifa hili.

Matapeli wa ardhi sasa wanataka kuuza jumba la Posta Nairobi, Nakuru, Eldoret, Mombasa na ile ardhi ya mahakama ya Karura. Wafanyakazi wanalazimishwa kutia sahihi na kukubali kuuzwa kwa mali ya wakenya. Anayetaka ardhi hizi hakika mwamjua kwa kilemba chake! Wakenya amkeni kumekucha Jubilee ni Paka wa duka la nyama. Hatosheki kula nyama.

Kila siku hakosekani dukani. Mbele ya muuza nyama ambaye ni wakenya hujifanya mzuri na mpole. Huyu paka hafai kusazwa tena. Anakula kwa dharau bila ya kuwajali wauza nyama. Kila kukicha ni dharau. Nilimtaja Raila Odinga kama Magufuli wa Kenya. Wengi walifoka na kunitusi. Narudia tena leo muungano wa NASA ni lazima iungane kuwaondoa hawa jamaa wa vituko. Dawa ya jubilee imepatikana.

Mohammed Ali. Kuwasiliana naye: FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Instagram: @mohajichopevu, Twitter: @mohajichopevu

Related Topics


.

Popular this week

.

Latest Articles