×
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The Standard Group is recognized as a leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national and international interest.
  • Standard Group Plc HQ Office,
  • The Standard Group Center,Mombasa Road.
  • P.O Box 30080-00100,Nairobi, Kenya.
  • Telephone number: 0203222111, 0719012111
  • Email: [email protected]

Jicho Pevu: Mabadiliko kwa mpigo ndiyo tiba ya Kenya

News
 Madaktari sasa hawaogopi kupigana tena na kuku wa kuchorwa ambayo ni serikali ya Jubilee. Hakika chuma chao ki motoni Agosti nane

Jinsi mambo yalivyo hapa nchini sasa, ni jukumu la kila Mkenya kusimama kidete na kukomboa Kenya.

Tatizo kubwa la taifa hili ni baadhi ya wakenya ambao kwa lugha ya kimombo wamepewa jina la Middle Class. Wakenya hawa ni wanafiki wakubwa kwani wao ndio wa kwanza kupiga domo na wa mwisho kukata kura au hata kupiga kura.

Hawa hujifanya kutosheka na maisha kwa sababu wana gari, mke mzuri, watoto na maisha mazuri — wamesahau kuwa asilimia kubwa ni ya wale wanao hangaika kutokana na udhalimu wa serikali hii. Habari njema ni kuwa waliojitenga sasa wameanza kuona adhari za kufyata domo.

Ijumaa hii ya neema naanza barua yangu na kutoa kongole kwa madaktari humu nchini.

Madaktari na CBA

Hebu na Mungu awabariki kwa kutoa mfano mzuri kwa wakenya waliojawa na woga wa kudai haki zao. Waakilishi wa madaktari walitiwa mbaroni kwa kudai haki zao lakini walichosahau serikali ni kwamba madaktari hao waliwafungua wakenya macho jinsi ya kutetea haki zao.

Madaktari sasa hawaogopi kupigana tena na kuku wa kuchorwa ambayo ni serikali ya Jubilee. Hakika chuma chao ki motoni Agosti nane. Huu si ungwana wala heshima.

Mamlaka ya mawasiliano CA

Hakika mwizi hana jina lingine ila mwizi. Ukiona mbwa anabweka mwenyewe, pasi na kusumbuliwa, jua huyo ni mbwa koko. Dalili za kushindwa kwa Jubilee zimeitia kiwewe kiasi cha kupanga kusikiza mazungumzo ya kila mkenya. Mimi nimezoea kusikizwa na serikali, lakini hii ya kutaka kusikiza hata mazungumzo ya bibi na bwana ni ushenzi wa hali ya juu.

Enyi wakenya mjue kwamba CA imeanzisha harakati ya kuzishurutisha kampuni za simu nchini ili kuruhusu vitengo vya kijasusi kudukua mawasiliano ya raia. Hatua itakayowapatia uwezo wa kudukua simu zinazopigwa, ujumbe na shughuli za kifedha. Hili si jambo geni kwa wanasiasa kwani NIS wamepiga kambi katika majumba hayo ya simu kusikiza simu za wanasiasa na wanahabari waliochoshwa na serikali hii ya ki-imla.

Iwapo watafaulu basi mpango huo utasababisha wakenya milioni 30 wenye simu kupoteza hali yao ya faragha pamoja na uaminifu.

Mahakama

Walioingia uongozini kupitia mahakama kuu sasa wamechoka na mahakama hiyo. Wameanza kuogopa maana wingu la mabadiliko Kenya limetanda, wezi wote sasa wanaogopa mahakama ya juu na ndio maana wanataka kupitisha mswaada kupitia bunge la matapeli kuafikisha wizi wa kura Agosti nane.

Na kwa vile wengi bungeni ni wale wale, basi huenda wakafaulu kuzima demokrasia. Lakini Agosti nane hamtakuwa na nguvu ya kuzima sauti ya wakenya zaidi ya milioni arobaine. Langu jicho tu!

William Ruto

Ndoa ya lazima imekaribia ukingoni. Mchumba mpya naarifiwa ni Gideon Moi. Wiki moja tu umefyata domo, wakenya wameanza kukuzungumzia, wengine wakikutaja kuwa uko hali mahututi huko Turkey. Ulipotokea watu walianza kuzungumzia afya yako. Hii ni makosa yenu viongozi.

Mbegu za chuki mlizopanda sasa hata wananchi wanawaombea mfe kwa machungu wanaopitia kwa niaba ya serikali yenu. Mimi nasubiri kuona jinsi talaka na ndoa mpya zitakavyoshamiri. Nilikuonya sasa tia chako maji.

Julius Karangi

Katika maisha yangu ya uanahabari nimekaa na jamaa huyu mara moja tu — alipokuwa katika afisi ya aliyekuwa waziri wa ulinzi wakati huo, bwana Yussuf Hajj. Kwa mtazamo wangu Julius Karangi alijifanya mzalendo na mpenda demokrasia. Alizungumzia masuala ya jeshi kama baba mpenda wanawe kumbe ni sura tu! Huyu ndiye jamaa aliyeingiza siasa ndani ya jeshi.

Naarifiwa hata wanajeshi hawampendi kwa madai ya uozo alioacha nyuma. Karangi sasa anataka kurudi katika siasa. Uthamaki unamsumbua na ndio maana ameamua kuendeleza siasa za Uhuru Kenyatta na William Ruto licha ya wawili hao kupofisha taifa na uongozi wao tasa.

Julius Waweru Karangi karibu kwenye siasa lakini ukumbuke wewe ni raia na wakenya hawatacheka na wewe tena. 2017 sio 2013!

Wakenya wafungwa

Sote tumekuwa wafungwa ndani ya taifa letu. Amkeni sasa, madaktari wametoa mfano. Wameenda jela na kutoka jela wakitetea haki zao. Hawawezi kutufunga sote, hawawezi kutudhulumu sote, hawawezi kutuangamiza sote.

Mimi nimeamua, mimi ninataka mabadiliko, mimi nimetolewa kafara, nitasema hivi karibuni lakini sitaogopa tena kulemazwa, sitaogopa kutetea taifa langu na watoto wa Kenya. Enyi mnaojiita middle class ni nyinyi tu ndio mliosalia tushinde hii vita.

Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN.

Kuwasiliana naye: [email protected], FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Instagram: @mohajichopevu, Twitter:

@mohajichopevu

Related Topics


.

Popular this week

.

Latest Articles

.

Recommended Articles