×
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The Standard Group is recognized as a leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national and international interest.
  • Standard Group Plc HQ Office,
  • The Standard Group Center,Mombasa Road.
  • P.O Box 30080-00100,Nairobi, Kenya.
  • Telephone number: 0203222111, 0719012111
  • Email: [email protected]

Jicho Pevu: Paruwanja ya mihadarati Kenya

News
 Ukweli wa mambo ni kwamba wanasiasa pamoja na serikali huitumia biashara kama njia ya kusafisha fedha haramu

Kenya inakabiliwa na tatizo la matumizi na biashara haramu ya dawa za kulevya.

Hali hii inachangiwa na mambo mbalimbali zikiwemo uelewa mdogo wa jamii juu ya tatizo hili, mmomonyoko wa maadili na tamaa ya kujipatia utajiri wa haraka. Urefu wa mpaka wa nchi zenye vipenyo vingi hurahisisha usafirishaji haramu wa dawa za kulevya na kufanya udhibiti kuwa mgumu.

Minghairi na matatizo haya yote, ni wazi kuwa dawa za kulevya haziwezi kuingia nchini Kenya bila baraka za serikali. Itakumbukwa wazi kuwa katika makala yangu ya Jicho Pevu — Paruwanja la mihadarati — miaka kama minane iliyopita, katika uchunguzi wetu wa kina tulibaini kuwa asasi za usalama, mahakama na viongozi wakuu ndani ya serikali pamoja na wanasiasa ndio waliokuwa wakifaidika pakubwa kutokana na mauzo ya dawa hizi haramu sio tu hapa nchini bali hata ulaya.

Maafisa wengi wa polisi waliuawa akiwemo Erastus Kirui Chemorei, DCIO wa bandari ya pwani Abdullahi Mohammed, maafisa wawili wa polisi wa utawala Juma Mwagatu na Badi Mwajirani miongoni mwa maafisa wengine wengi wa polisi waliouawa kinyama kwa ajili ya kupambana na madawa haramu nchini.

Ukweli wa mambo ni kwamba wanasiasa pamoja na serikali huitumia biashara kama njia ya kusafisha fedha haramu. Fedha hizi huchangia pakubwa mfumuko wa bei, kuhodhiwa kwa uchumi na watu wachache, ongezeko la pengo la vipato na kuwepo kwa uwekezaji haramu.

Serikali zinazojihusisha na madawa za kulevya hufanya hivyo sio kuwalemeza wenyeji kwa kuwauzia hadharani kama njugu karanga, ila kwa kufaidi kupitia mzunguko wa fedha haramu al-maaruf Money Laundering.

Sasa nauliza tu, je, ni nani muuzaji mihadarati nchini? Mimi kama mwanahabari niliyezamia suala hili kuanzia, Malindi, Mombasa, Nairobi, Kitale, Uholanzi hadi Ubelgiji — na kufanya uchunguzi wa kina — naweza sema wazi bila woga kuwa muuzaji nambari moja wa mihadarati Kenya ni nani!

Vita dhidi ya Islamic Party Of Kenya (IPK)

Baada ya serikali ya Daniel Toroitich Arap Moi kuona nguvu za chama hicho mjini Mombasa, serikali ya Marekani ilichukua fursa hiyo kuvunja vunja matumaini na imani ya dini ya wana-pwani.

Walianza kuhakikisha kuwa mambo ambayo yalikuwa yakipingwa na imani za dini ya ki-islamu zimepewa kipau mbele. Vyumba vya anasa vilianza kuongezeka, mavazi yakaanza kubadilika, ushoga ukaanza kukubaliwa, miraa, pombe, dawa za kulevya zikaanza kuwafikia watoto wa Mombasa.

Pole pole wakaanza kusahau dini, utamaduni na heshima kwa wazee. Mombasa tulivu ikageuzwa jina na kuitwa Mombasa raha. Raha ikawateka nyara wana-pwani kiasi cha kuongeza majeneza kila kukicha. Marekani ilidhani imeshinda vita hivyo kwa kuhofia chama hicho cha waislamu kuboresha uislamu lakini ilichosahau sawia na vita vya kigaidi wao huchokoza na baadaye kujipata wao ndio wenye hasara kubwa.

Dawa zilienea na kuua watoto wetu lakini biashara hiyo iliingiliwa sasa na watu waliokuwa wakitaka kuua pia watoto wa wa-marekani. Kizazi kipya cha walanguzi kilizaliwa.

Ibrahim Akasha Abdalla

Huyu ndiye baba yao katika biashara hii. Kabla ya kuuawa kwake huko Uholanzi katika barabara ya Blood Straat Amsterdam, Ibrahim Akasha aliteka nyara biashara hii na kuanza kuangalia soko ya dunia. Alilenga Marekani na Ulaya kuhakikisha kuwa amejifanikisha ki-maisha na kujiita mfalme wa dawa za kulevya duniani baada ya majina mazito kama Pablo Escobar.

Ibrahim Akasha alijitajirisha, kuoa wake wawili na kupata vizazi vya kumridhi. Yeye binafsi alikuwa akimpenda sana Baktash Akasha kwa maana walifanana sana na alikuwa na tabia kama zake. Amerika ikidhani imevunja vunja IPK na kulemaza dini ya ki-islamu dawa zilianza kuwamaliza watoto wao. Hata baada ya kufa kwa Ibrahim Akasha biashara ilizidi kunawiri huku serikali zote husika za hapo awali — na sasa kwa njia moja au nyengine zikisaidia kisiri na kujifaidi huku watoto wetu wakiangamia.

Sasa Marekani inalia, Kenya inalia kwa kejeli, Kenya imejaa ufisadi haiko tayari kupigana na dawa za kulevya kwa sababu ufisadi ndio chakula chao cha mchana. Enyi wakenya wenzangu, naomba mnionyesha afisa mmoja wa serikali atakayekataa hongo ya shilingi bilioni mbili kutoka kwa walanguzi. Mkipata mmoja basi nitaamini hivi vita tutashinda sote!

Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN. Kuwasiliana naye: [email protected], FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Instagram: @mohajichopevu, Twitter-@mohajichopevu

Related Topics


.

Popular this week

.

Latest Articles