×
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The Standard Group is recognized as a leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national and international interest.
  • Standard Group Plc HQ Office,
  • The Standard Group Center,Mombasa Road.
  • P.O Box 30080-00100,Nairobi, Kenya.
  • Telephone number: 0203222111, 0719012111
  • Email: [email protected]

Kura na twafa njaa jamani?!

News
 Ekornop Lotieng apumzika kwake katika kijiji cha Nukulumei Turkana kaskazini. Tunaabudu kura kuliko uhai!

Picha huzungumza maneno mengi kuliko maneno yenyewe. Picha inayozungumzwa sana wiki hii ni ya kibonzo. Kibonzo kilichochorwa gazetini. Picha ya binadamu akiwa kalala, yuafa kutokana na njaa. Yuafa kutokana na ukame. Ilhali mbele yake ni mwanaIEBC akitaka tu kumsajili kuwa mpiga kura. Mbele yake ni mwanasiasa. Akitaka tu ajisali kuwa mpiga kura. Basi!

Hata vilabuni, hotelini, kila mahali, waambiwa ujisajili mwanzo ndio upate huduma unayohitaji. Tunaabudu kura kuliko uhai! Tunaabudu uchaguzi kuliko utu! Labda ndio maana baadhi ya viongozi wanatoroshwa na kukemewa katika mikutano ya siasa.

Kwa kuwa wanasema mambo yayo hayo kwa yayo. Propaganda zile zile za Abunuwasi. Za hamwoni barabaraba? Za hamna stima? Ilhali anayeulizwa hajatia kitu mdomoni siku ya ngapi sijui vile.

Ulitarajiwa uwe mchakato wa Wakenya kujisajili kuwa wapiga kura. Lakini umegeuzwa mikutano ya siasa, kampeni na kujifaragua. Halafu ajabu ni kuwa mwisho wa siku idadi ya wanaojisajili inazidi kupungua badala ya kuongezeka! Wajisajili vipi kupiga kura ilhali mshindi na mshinde wanajulikana tayari! Waingia vipi uwanjani kucheza na tayari timu pinzani ishapewa mabao mawili na mwamuzi! Niwaambie hivi viongozi wa upinzani na serikali waliomo mbioni kutuomba kujisajili kuwa wapiga kura, ili tuwarejeshe mamlakani Agosti wazidi kutuibia na kula.

Mwanzo hali ya uchumi nchini ni mbaya sana. Bei za bidhaa muhimu zimepanda vibaya vibaya, kiasi kwamba unga wa sima ni ghali kuliko wa chapati! Leo hii kumudu kununua sukuma ya shilingi kumi ni muujiza! Maji hayapo. Ukiufungua mfereji wa maji wakoroma kama nguruwe anayechinjwa vile!

Nguvu za umeme ni mgao kwa mgao. Lakini bili za maji na nishati ni sawa na kumnunua kifaru na kipusa! Wenzetu wanauliwa kutokana na baa la njaa. Mifugo inamezwa na ukame. Hali ya uchumi imedorora pakubwa. Lugha iliyopo sasa ni RETRENCHMENT na COST-CUTTING!

Enyi waomba kura njooni mikutanoni na magalani ya maji na slesi za mikate. Njaa yatuua maskini! Tumecharara. Twanuka umaskini na njaa jamani! Migomo imezoeleka hadi vyombo vya habari havifuatilii tena. Migomi imekuwa hali ya kawaida. Si madaktari, si wauguzi, si walimu, si wahadhiri. Imebaki tu nchi kuuzwa kila mmoja apewe haki yake.

Twende wapi jamani? Mashambulizi ya Al-Shabab je? Halafu wewe ni kuniimbia tu kura. Kwani wataka kura zenyewe upigiwe na mfu jamani? Po! Wakenya tumechoka! Miye sitokimya, je wewe? Ni kura au kula?

Hassan mwana wa Ali ni Mhariri wa Michezo na Nahodha wa Nuruyalugha (RADIO MAISHA).

[email protected], [email protected], FB: Ali Hassan Kauleni, Hassan mwana wa Ali,Twitter: @alikauleni

Related Topics


.

Popular this week

.

Latest Articles