×
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The Standard Group is recognized as a leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national and international interest.
  • Standard Group Plc HQ Office,
  • The Standard Group Center,Mombasa Road.
  • P.O Box 30080-00100,Nairobi, Kenya.
  • Telephone number: 0203222111, 0719012111
  • Email: [email protected]

Jicho Pevu: Uhuru Kenyatta kubali yaishe!

News
 Rais Uhuru Kenyatta Picha: Hisani

 Mnataka nifanye nini? Hii ndio kauli ya Uhuru Kenyatta kwa wakenya. Wakenya waliomchagua pamoja na waliompinga vikali katika chaguzi tata ya mwaka wa 2013 iliyoamuliwa na mahakama ya Jaji mstaafu Willy Mutunga.

Leo jamaa aliyekuwa akipigania uongozi huo ameambulia kujua kuwa uongozi ni nyota sio jina. Uongozi ni kujitolea sio sifa za mitandao.

 Uongozi wa taifa una tofauti kubwa sana na uongozi wa vijijini. Leo jamaa aliyekuwa akijizatiti na manifesto yake ya mwaka wa 2013 na ahadi chungu nzima amesalia kuwa kama mpita njia kwani ameishia kuwarudia wale wale aliowaomba kazi na kuwauliza afanye nini kwa kazi waliompa maana ni kana kwamba imemshinda.

 Uhuru Kenyatta kama hujui la kufanya nitakwambia la kufanya bila kuogopa makabila yanayokuabudu. Jiuzulu! Fanya maamuzi ya hekima na uJiuzulu maana kazi ya kuwa kichwa cha taifa kimekushinda.

Unayojua sasa ni hasira na kujibizana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa kukuambia ukweli. Katika kongamano lako huko Bomas umethihirishia wazi wakenya kuwa wewe hustahimili na huna subira.

Maneno yaliyokutoka kinywani katika ukumbi wa Bomas sio maneno ya kiongozi. Kumtusi Raila Odinga na kumlimbikizia lawama mbele ya muungano wa makabila mawili si haki wala demokrasia.

Sio uongozi wala mfano wa kuiga, ila ni dharau na dalili ya uongozi kukushinda. Kama msomi na mwanahabari, matamshi yako huko Bomas yalikuwa matamshi ya kunoa makali ya kabila yako na ya Naibu wako kuungana zaidi na kuona makabila mengine yanayopinga uongozi wako uliofeli kama makabila nyoka.

Muungano wa makabila mawili kuendelea kuamini kuwa makabila hayo tu ndiyo yaliyo na nyota ya kuongoza taifa hili.

Muungano wa kuunga mkono wizi wa mali ya umma badala ya kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya walioibia wakenya.

 Bwana Uhuru Kenyatta hili halitapasi kamwe maana wakenya wamekomaa. Hata wanaotoka katika kabila lako washajua wazi kuwa kazi imekushinda.

Wanalia biashara zao kuzama, wanateta kila kukicha japo kimya kimya. Kabila la pili uongozi pia wanajua wazi kuwa ipo siku mtaamua kuwanyoa kwa chupa bila maji.

 Wanajua vyema hamna mkikuyu atakaye muunga mkono William Ruto. Wanajua hizo ni hekaya za abunuasi. Kwa rafiki yangu William Ruto VINYOZI wa mlima Kenya wanakusubiri.

Siku miungu yao itasema wewe ni nyoka basi jitayarishe kupigwa mawe. Siku hiyo yawadia! Kinachonifurahisha zaidi ni kuwa wakalenjin wanajua wazi kuwa ndoto ya William Ruto ni tasa na haitaoteka.

Ruto kwa upande wake bado ni mjanja kiasi japo ndege mjanja hunaswa kwa tundu bovu. Kuundwa kwa chama cha LPK na Ababu Namwamba kutumiwa ni ishara tosha kuwa LPK ni William Ruto, Ababu Namwamba ni kondakta tu.

William Ruto anajua wazi kuwa ndoto ya kuungwa mkono na mlima Kenya ni porojo tu na ndio maana ameanza kujipanga na mapema. Iwapo jubilee itatoa ushindi mwaka wa 2017 japo hilo ni kama kukamua mende maziwa basi milango ya jela dhidi ya William Ruto itafunguliwa.

Jamii inayomdang’anya sasa itamsulubu hadharani na kumwita majina hiyo siku. Rafiki yangu William Ruto kaa macho! Nikirudia ya Uhuru Kenyatta, bado nasisitiza ajiuzulu maana atazidi kujiaibisha na kuabisha wakenya waliokuwa wakiamini yeye ndiye suluhu la taifa hili.

Hila na gilba za Jubilee hazitafua dafu mbele ya Wakenya. Bwana Uhuru Kenyatta, taifa haliendeshwi kwa mtandao, densi au picha za hapa na pale. Taifa haliendeshwi na hasira au kujipiga kifua. Taifa linaendeshwa na hekima pamoja na mapenzi tele.

Leo wakenya wanaumia kwa sababu ya ufisadi chini ya uangalizi wako. Serikali yako chini ya uongozi wako ndio sasa serikali fisadi tangu Kenya kujinyakulia uhuru. Leo ufisadi umebisha hata kwa familia yako kiasi ya wakenya kujua sura zao.

 Leo watu wanaiba hata pesa za wagonjwa, pesa za dawa za ukimwi. Jameni ni nini serikali hii yako haiwezi kuiba? Nahofia kilichosalia kuibiwa sasa ni ramani ya taifa maana wewe pamoja na viongozi wengine ndani ya serikali yako mnaonekana kutokuwa na ukenya ndani ya mioyo zenu.

Babako hayati mzee Jomo Kenyatta licha ya hata kutohusika zaidi na kupambana vikali na wakoloni kama walivyofanya kina Field Marshal Dedan Kimani aliishia kujipatia ardhi kubwa na kutawala kwa kifua.

 Leo umerithi historia ya babako, kuanzia bendera uliochagua ya urais, hotuba za marehemu babako na hasira za mkizi.

Alichotuambia babako miaka ya nyuma ndio unachotuambia sasa. Amka kumekucha Uhuru Kenyatta. Kenya sio Kenya ya zamani ya baba na mama. Kenya ni ya kila mkenya na wakenya wana haki ya kuuliza haki na ushuru wao.

 Usitishe wakenya eti mtatawala hadi mwaka wa 2022! Kwani mtajipigia kura nyinyi mnaotisha watu na uongozi? Kama uongozi umewashinda jiondoeni kabla hamjaondolewa.

Someni historian a mjue hamna nguvu zaidi ya waliowengi hata kama jeshi na polisi ni zenu.

Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN. Kuwasiliana naye: [email protected], FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Instagram: @mohajichopevu, Twitter: @mohajichopevu

Related Topics


.

Popular this week

.

Latest Articles