
Wakati ukuta. Wakati wenyewe unakimbia.
Hivyo unavyokimbia wakati ndivyo yanavyokimbia maisha. Na maisha kila yakikimbia, nao umri ukitimka. Ndio hapo mwalimu Wallah BinWallah husema siku zote: “Aliyelala aamke, naye aliyeamka atimke, na kwa yule ambaye kwamba keshatimka afike.”
Likizo ‘fupi’ ya mwezi Agosti imetimka. Imefikia kikomo. Sasa ndio hivi tena tupo katika mwezi wa Septemba. Ishara tosha kuwa vijana wetu wamekwisha kurejea shuleni kupambana na muhula wa tatu.
Ni yetu maombi na matarajio kuwa muhula huu utakuwa na neema. Yaani Mola Atatuepusha na majanga na mikosi ya mioto iliyozua vurugu na uharibifu mkubwa wa mali. Na hapo kutatiza pakubwa kalenda ya masomo nchini. Atokomee mbali kusikojulikana pepo huyo mbaya! Semeni nyote ashindwe!
Huu ni muhula wenye shughuli nyingi tu. Kubwa ikiwa ni mitihani. Mitihani ya ama kufanikiwa kuingia darasa jingine kama ni shule ya upili, kidato kingine kama ni sekondari au daraja jingine kwa wanetu walioko katika vyuo na taasisi za elimu ya juu.
Hata hivyo, kikubwa muhula huu wa tatu na wa mwisho mwaka huu ni mitihani ya taifa ya darasa la nane au kidato cha nne. Ndio hapo nikaamua kusema na wanafunzi wetu.
Watahiniwa wetu wanahitaji sana utulivu na amani wakati huu wa mitihani ya taifa. Matumaini yetu sote yakiwa kuwa mazingira haya matulivu yataendana na watahiniwa wetu kufanya mitihani ya halali, kupata matokeo ya halali na kuishi maisha ya halali.
Kwa kifupi ni kuwa hatutarajii kushuhudia visa vya wizi wa mitihani kama ilivyokuwa mwaka jana baada ya kutangazwa matokeo ya mitihani ya taifa.
Vijana wetu. Wanafunzi wetu. Nawaita na kusema nanyi kwa utulivu na unyenyekevu: Sikilizeni maneno haya. Mtanikumbuka siku zenu za uzeeni. Ujana ni kama moshi na ukienda haurudi tena. La kwanza hilo.
Pili, na ndilo muhimu mno, kumbukeni kuwa maisha ni ghali mno. Kupata karo zenu wazazi wenu wanavunjika migongo. Wanadaiwa kope si zao. Mikopo hata usiseme. Kununua zana za shule ni ghali mno. Usiseme vitabu na viatu. Nauli yenu kurudi shuleni inabidi tukope jamani.
Kwa maana hiyo nawaomba kitu kimoja: Mtuonee huruma siye wazazi wenu. Nendeni shuleni mkasome. Huu ni muhula wa kubukua jamani. Hatutaki mara mwafulani kavunja nini, mara nani kafanya nini vile. Tupeni muda wa kuwatafutia mahitaji na masrufu mengine. Muda wa kuja shuleni kila mara kutatua migogoro wacheni tuwatafutie karo jamani.
Zingatieni masomo. Zawadi yenu kwetu ni kufanya vema katika mitihani. Tunawaomba mturidhishe ‘balaa’ nzuri za kuwatafutia karo kujiunga na shule za upili na vyuo wala sio ‘beluwa’ za kutatua zahama shuleni, au siyo?
Wapeni walimu na wahudumu wengineo shuleni wakati mzuri. Ushirikiano ndio maendeleo. Kichango kuchangizana wanafunzi wetu jamani.
Wanafunzi na watahiniwa wetu wote twawatakieni kila la kheri muhula huu. Mola Awabariki. Kumbukeni kuwa siku zote cha jasho hakikosi utamu. Vivyo hivyo wazazi, ndugu, jamaa na marafiki wanawatakieni kila la kheri. Mvune ya kheri wala sio ya shari. Msisahau kuwa mvuna janga hula na wa kwao.
Hassan mwana wa Ali ni Mhariri wa Michezo na Nahodha wa Nuruyalugha (RADIO MAISHA).
[email protected], [email protected], FB: Ali Hassan Kauleni, Hassan mwana wa Ali, Twitter: @alikauleni