×
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The Standard Group is recognized as a leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national and international interest.
  • Standard Group Plc HQ Office,
  • The Standard Group Center,Mombasa Road.
  • P.O Box 30080-00100,Nairobi, Kenya.
  • Telephone number: 0203222111, 0719012111
  • Email: [email protected]

Nairobi imeoza jamani

News
 Msongamano wa magari jijini. Picha: Hisani

Cheza na moshi ukohoe!

Yaonekana wazi kuwa wakazi, wazawa na wadau wengineo wote – wawe ni watalii, wafanyi-biashara, wawekezaji hata wapita-njia tu – katika jiji kuu nchini Kenya, Nairobi, tulicheza na moshi mwaka 2013 kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu nchini Kenya. Viongozi wa jiji la Nairobi wamekuwa na utendi-kazi duni sana!

Ni kutokana na ubovu na utepetevu huo katika uongozi ndio maana sasa hivi kila 'mmoja' amejitokeza kimasomaso kutangaza azma yake ya kutaka kuwania kuwa ama gavana, seneta, mwakilishi wa wanawake, mwakilishi wa wadi na nyandhfa nyinginezo katika uchaguzi mkuu ujao.

Almradi kila 'mtu' anawania kuongoza Nairobi. Kisa na maana ni kutokana na uongozi mbovu. Lakini kikubwa ni kuwa jiji la Nairobi ndilo lililo na mgao mkubwa kutoka kwa serikali kuu. Na ndicho kituo cha uchumi wa taifa hili. Senti zipo Nairobi ati!

Wiki mbili hivi zilizopita nikiwa napiga malapa katika jiji la Mombasa na swahibu yangu Mohammed Raj aka Annam aka mvuvi halisi aka Diwani Mtarajiwa, niliajabia Mombasa! Mbali na matatizo yake ya hapa na pale, Mombasa sasa hivi ni mji safi jamani. Hongereni Wapwani!

Sasa turudi Nairobi. Vijia, vichochoro na vishoroba vya Nairobi vyanuka fe! Taka pembe zote. Wachuuzi – wenye makeke, lugha ya kubembeleza, ukemi na kila aina ya fujo – wametawala jiji ni kama nzi kwenye kidonda! Kutembea kwa miguu ni miujiza!

Matatu 'zinapakia' na 'kupakua' abiria kila kona ya jiji la Nairobi, sikwambii kelele na zahama za utingo, madereva wasiojua be wala te kuhusu sheria za barabarani!

Hapa tungesaidiwa na maafisa wa polisi wa baraza la jiji: Kanjo. Hao nao usiseme. Hujificha badala ya kuelekeza. Wakajitokeza ghafla 'kutoza ushuru' na kuwabughudi wakazi wa Nairobi. Magari yao makweche kama nini yamejaa ovyo barabarani. Ndani ya magari hayo 'wahalifu' wakitozwa ushuru. Nairobi jamani!

Msongamano wa magari nao? Wakumbuka jiji lilivyokuwa alivyokuja nchini mwezi jana Waziri Mkuu wa Israel Benjamin "Bibi" Netanyahu? Vipi mwezi huo kulipoandaliwa Kongamano la Kimataifa la Maendeleo na Biashara? Barabara "zote" zilifungwa pasina kuwepo plan B. Ikabidi rafiki yangu Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyi-kazi, COTU, ndugu Francis Atwoli kuwaita 'washenzi hao'.

Kutoka mji wa Kisumu hadi Nairobi kwenye ndege ni muda wa nusu saa tu! Kisha kutoka uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta hadi katikati ya jiji wachukua saa mbili!

Wafanyi-biashara wanatatizika kila mara kutokana na mgao wa nguvu za umeme! Hadi lini jamani? Kupata maji katika mifereji ya jiji la Nairobi ni muujiza! Maji ni lulu. Tembea leo hii katika mitaa ya Umoja, Donholm, Kasarani, Buruburu...utanijibu yakhe.

Uhaba huo wa maji na nguvu za umeme waendelea huku nasi makabwela tukilipa bili nono kila mwisho wa mwezi! Ewe! Nairobi jamani! Aisee natamani vijijini.

Leo hata nisizungumzie hali ya usalama na bei za bidhaa. Tutalizana bure!

Seneta Mbuvi Gideon Kioko aka Sonko umeonekana UKIJARIBU. Lakini bado. Ungeshirikiana na gavana? Labda

Gavana Mike Evans Odhiambo Kidero uliahidi mengi tu jamani. Miye siombi mengi. Naomba tu mawili ambayo umeyafanya.

Haki jiji la Nairobi lachukiza. Swala ni je, limeoza?

Hassan mwana wa Ali ni Mhariri wa Michezo na Nahodha wa Nuruyalugha (RADIO MAISHA).

[email protected], [email protected],

FB: Ali Hassan Kauleni, Hassan mwana wa Ali,

Twitter: @alikauleni

Related Topics


.

Popular this week

.

Latest Articles