×
The Standard Group Plc is a multi-media organization with investments in media platforms spanning newspaper print operations, television, radio broadcasting, digital and online services. The Standard Group is recognized as a leading multi-media house in Kenya with a key influence in matters of national and international interest.
  • Standard Group Plc HQ Office,
  • The Standard Group Center,Mombasa Road.
  • P.O Box 30080-00100,Nairobi, Kenya.
  • Telephone number: 0203222111, 0719012111
  • Email: [email protected]

Mohammed Ali's Jicho Pevu: Raila Odinga ndiye Magufuli wa Kenya

 Tanzanian President Pombe Magufuli (L) and Cord leader Raila Odinga

Nasema bila woga wala shauku yeyote kwamba Kenya yahitaji Magufuli wake.

Tulionao kwa sasa sio Magufuli ila matatizo. Wakati ambapo Magufuli anafungua kufuli zote Tanzania, uongozi wa Uhuru Kenyatta unaendeleza uhuru wa ufisadi Kenya.

Sifa za Magufuli toka alipotwaa uongozi wa Tanzania zimewafikia hata wakenya. Wengi wamemsifu na wengine wameandika wakiomba Mungu awape rais kama Magufuli.

Kwa kipindi kifupi alichoingia madarakani, Rais Dkt John Magufuli amefanya mambo kadhaa ambayo yamewaridhisha na kuwapa moyo Watanzania. Mambo hayo ni kama, ziara yake ya ghafla katika hospitali ya Taifa la Muhimbili, ambapo alifuta bodi ya wakurugenzi wa hospitali hiyo pamoja na kumuondoa kaimu mkurugenzi wake.

Kufuta safari za viongozi kwenda nchi za nje ili kupunguza matumizi makubwa ya pesa za serikali, kuelekeza shilingi milion 225 zilizochangwa kwa ajili ya kugharamia hafla ya Pongezi za Wabunge Dodoma kutumika kununua vitanda vya hospitali — Shilingi milion 15 tu ndizo zilizotumika kwa ajili ya sherehe hiyo.

Jumatatu ya tarehe 23 November 2015, Magufuli alitangaza kufuta kwake kwa siku kuu ya Uhuru inayoadhimishwa December 9, na kuagiza fedha za maandalizi ya siku hiyo zitumike kutatua matatizo mengine. Pia ameagiza siku hiyo itumike kusafisha mazingira ili kupunguza matatizo ya kipindupindu nchini.

Huyu ndiye Rais mtajika wa Tanzania ambaye huwezi kumlinganisha na wengi haoa Africa akiwemo wetu.

Sisi hapa twaonyeshwa vihoja vya ukatuni bila kujali maslahi ya wananchi. Wetu hapa wamekuwa mafisi, hata maombi haiwezi kuwasaidia kwani sikio la kufa halisikii dawa.

Dawa ya hawa makabwela ni moja tu! Wakenya wakubali sura ya kutuongoza, lakini nyuma ya sura hii tuwe na vijana chipukizi wana mabadiliko watakao kaa macho kwa kila maamuzi ya taifa hili. Je, sura ni nani?

Sura ya Magufuli Kenya ni Raila Odinga. Kenya sasa yahitaji Raila kuchukua ushukani na kuikomboa Kenya kutoka kwa vijana toka kwa janga la Jubilee.

Kukwamua taifa toka kwa uongozi ulioibaka demokrasia ya wakenya na Kenya kwa jumla.

Viongozi hawa wana sera ni zile zile za ukandamizaji na ya kihayawani — hamna kujali raia wake.

Enyi wakenya wapenda amani someni historia ya taifa hili. Waskizeni wazee na hivyo mjaribu kufungua macho muweze kuonae kila kitu kwa jicho la tatu, wala sio jicho la ukabila.

Nani asiyejua kwamba historia ya Kenya haiwezi andikwa sahihi bila kuwepo mchango wa Raila? Uhuru Kenyatta na William Ruto hawapo kamwe kwenye historia ya kenya.

Kama ni historia basi kwa hawa wawili ni historia ya dhulma na ufisadi wa hali ya juu waliorithi toka kwa mababu zao ambao kila mkenya anawafahamu.

Leo Rais Uhuru Kenyatta amekuwa kama waziri wa mambo ya nje, sio rais tena, huku naibu wake Ruto akiwa kama mlinzi.

Someni historia jameni! Na ndio maana ningelipenda kutaja kwamba historia itakapoandikwa kuhusu maendeleo na upanuzi wa demokrasia nchini Kenya, Raila Odinga atatengewa sura nyingi.

Sura za shujaa na mpenda kenya aliye na utaifa ndani yake. Kiongozi aliyepigana vita mamluki na wafisadi wakubwa nchini.

Huyu ndiye Magufuli wa Kenya mwaka wa 2017. Hulka yake ni kubainisha mbivu na mbichi. ukweli huu umedhihirika wazi tunaposoma historia kuhusu waanzilishi wa taifa hili waliojitahidi sana kuikomboa Kenya kutoka utawala dhalimu wa wakoloni.

Historia huzama zaidi za kuonyesha mchango wa kila mmoja kwa namna inayotuchorea taswira ya mwono-ulimwengu wa kila mmoja.

Lakini kwa kuwa historia ni tundu, inafumbata mambo haya kwa uketo wa kuajabisha sana.

Je, ni funzo gani ambalo Raila Odinga anapaswa kupata kutokana na misukosuko ya mawimbi ya siasa ambayo amepitia katika kipindi chake kirefu cha miongo kadha ya siasa za ukombozi?

Raila sasa anafaa alegeze kamba na kuwakubali vijana kuingia ndani ya chama chake na kuongeza nguvu ya kupambana na mafisadi. Ni sharti Raila akubali kushirikiana na vijana, awape nafasi, mawaidha kisha akae kando aone vile ambavyo vijana hao watakomboa kura zake zote.

Bila ya vijana, Raila hataenda popote. Wanaomzingira Raila wafaa wamweleze haya bila woga, wamweleze afungue mlango wake wazi na aache vijana wanaotaka kumsaidia kuchukua uongozi kufanya hivyo ki-demokrasia bila ya wao kunyimwa nafasi za kufanya hivyo.

Hii ndio silaha ya mwisho yake Odinga. Amekuwa ni jabali anayehitaji vijana kufanikisha ndoto yake ya kuwakomboa wakenya.

Sifa zake zinazidi kubobea kila kukicha. Anachohitaji sasa ni kuongeza makali na damu mpya ndani ya chama chake. Damu moto ya vijana wanaotaka mabadiliko kwa mpigo mmoja tu.

Punda amechoka, na vijana pia wamechoka! Ifahamike wazi kuwa mtu huzaa neno. Neno hilo likawa kubwa kumzidi mtu huyo aliyelizaa na hatimaye likambwaga.

Ninaamini kwamba siku moja, ndoto za Raila Odinga hazitakuwa ni ndoto tu – bali ukweli mtupu. Ukweli ambao labda wengi wanaogopa kuusema ni kwamba demokrasia ya Kenya itamaskinika bila Raila Odinga kushika usukani wa kisiasa nchini Kenya.

Wasemavyo waswahili heri kafiri akufaae kuliko silamu asiyekufaa na zimwi likujualo halikuli likakumaliza. Ya Jubilee tumeona na hatutakikusikia tena. Kelele zao za kusema na kutenda na waziseme wakiwa nje ya ikulu mwaka wa 2017. Historia itajiandika tena mwaka wa 2017.

Kenya yahitaji Magufuli wake wa tangu mwaka wa 2007 na 2013, na huyo ni Raila. Kwa viongozi mnaoongoza kwa misingi ya kikabila, mfahamu zenu zimefikia kikomo.

Enyi wakabila wakubwa mnaoongoza kwa ukabila kumbukeni Raila hakuwa mwendawazimu aliposema Kibaki Tosha licha ya kujua fika Mwai Kibaki siyo mjaluo. Pili, hata baada ya kufahamu fika alivyofanywa babake Jaramogi Oginga Odinga miaka ya nyuma, yote aliyatupa katika kaburi la sahau na akatizama taifa na utaifa.

Je, hapakuwa na makabila mengine? Je, mkikuyu na mkalenjin mgani leo yupo tayari kusema Raila tosha? Kama yupo jawabu asinipe lakini alitoe 2017.

Mohammed Ali ni Mhariri Mkuu wa Kitengo cha Upekuzi KTN. Kuwasiliana naye: [email protected], FB: Official Jicho Pevu with Mohammed Ali, Twitter: @mohajichopevu

 

Related Topics


.

Popular this week

.

Latest Articles