Majuzi katika kongamano la kitaifa la mchakato wa kuunganisha nchi al maaruf BBI (Building Bridges Initiative) kule Bomas, Nairobi kulizuka mgeni wa nchi jirani aliyehutubu na kuacha maswali mengi kwa wadadisi wa kisiasa.
Bwana huyu ni Waziri wa mambo za nchi za nje wa Tanzania Profesa Palamagamba Kabudi. Sambamba na hulka na sifa za watanzania alitowa hotuba ilosheheni ukwasi wa lugha teule ya Kiswahili na mahanjam mengi ya kiabunuasi. Akibwabwaja kama cherahani ya Mjerumani mfano wa baba yao wa taifa Julius Nyerere bwana huyu mwenye macho makubwa ya kung’ara kama bundi ama paka mwanga alisema mengi ambayo ni ya kutatanisha.