Uhuru amtoa Kalembe Ndile ndani ya baa

Mwanasiasa Kalembe Ndile.

Mwanasiasa mcheshi Kalembe Ndile ni mtu wa kawaida. Sawia na nguo ya kaniki, kamwe huwezi kumbadilisha jinsi alivyo kimazungumzo, maisha yake, msimamo wake katika kila jambo analonuia ama msukumo wowote unaokadiria kumyumbisha.

Bado haijulikani iwapo wazo ama hatua ya serikali ya Uhuru Kenyatta kumkumbuka mwanasiasa Kalembe Ndile pamoja na wenzake wa Ukambani kuteuliwa wakurugenzi wa mashirika hivi majuzi ni kutokana na huruma, malipo ya hisani ama msukumo kwamba rafiki ya Kalembe Ndile anachomwa na jua kali la pwani akihudumia wateja kwenye mkahawa wa mvinyo.

Maisha yalipoanza kumkalia magumu alianza kulalamikia serikali ya Jubilee jinsi ilivyomtupa kama jongoo na kijiti chake baada ya kuwalemaza wenye vyama vidogo ambao walijitoa mhanga kuvimaliza kwa sababu ya muungano wa Jubilee.

Alisubiri kuona kama ataweza kuzawadiwa kazi kama walivyoahidiwa wote wakati walipoenda kuzika vyama vyao vya kisiasa katika Ikulu ya Nairobi mwaka 2017.

Kwa bahati nzuri ama mbaya, Rais Uhuru na naibu wake Ruto wakarejea serikalini lakini ikawa na mabonde na milima ya kisiasa hususan kufuatia kuingia kati kwa kiongozi wa NASA ama upinzani Raila Odinga hivyo matarajio ya kina Ndile na wengine yote yakadidimia.

Kalembe alivyoona hali hiyo, aliwajibika kutafuta kazi yoyote ile mradi maisha yatajikokota kwake. Alifufuliza mno kwa kaka yake na rafiki gavana wa Nairobi, Mike Mbuvi Sonko ambaye twaambiwa alimuonea huruma mno na akaona badala ya mtu mzima kumwajiri katika idara yake ya SONKO RESCUE TEAM, ni bora amweke katika mkahawa wake wa baa.

Kwa muda sasa, Mheshimiwa Kalembe Ndile amekuwa mhudumu wa baa akiwapokea pia wageni wanaomtembelea gavana Sonko anapokuwa kwake katika maskani ya Kikambala, Kilifi. Habari hizi huenda zikawa zilimfikia Rais wa Jamhuri ambaye aliamua kumtoa Kalembe Ndile kutoka ndani ya baa hadi kuwa mkurugenzi wa shirika la Tanathi kwa kipindi cha miaka mitatu.

Hii ndio iliyokuwa ndoto ya mwanasiasa huyu kitambo chote kile ambacho amekuwa akisononeka kimoyomoyo kila anapokutana na wanasiasa wenzake wanaomtembelea gavana Sonko nyumbani kwake Kikambala ambao wengi humshangaa kumkuta hapo.

Hivi tuzungumzavyo, ni miongoni mwa wanasiasa wa ukambani ambao Rais Uhuru Kenyatta aliwaonea huruma kwa kuwateua wakurugenzi wa mashirika mbali mbali ya serikali kote nchini baada ya kusurunda tangu kutaifisha vyama vyao vya kisiasa wakijumuika kwa chama cha Jubilee.

Kalembe ndile akiwania kiti cha ubunge na chama chake cha Tip-Tip

Kalembe Ndile ni mmoja wa wenye vyama vya kisiasa ambapo aliamua kukitia kitanzi chama chake kilichomfaidi kwenye uchaguzi mkuu wa 2013 cha Tip Tip kwa ajili ya kuwaunga mkono Rais na naibu wake kwa uchaguzi wa 2017.

Yeye alionelea badala ya kurudi Kibwezi West tena 2017, alijua mambo kule huenda yakawa mabaya zaidi kuliko yale 2013 alipoangushwa kwenye uchaguzi wa ubunge mfano wa sufi. Hivyo alipozika chama chake, akaamua kuwania ubunge wa eneo bunge la Mavoko ambako aliangushwa sawa na vile unavyoona yai la kuku linavyoanguka.

Kulingana na marafiki wake wa karibu, kuanguka kwake kiti cha Mavoko na kuzika chama chake cha TIP TIP kwa Jubilee, maisha yake ya kawaida nay ale ya kisiasa yalimgeukia kuwa ya “Zanga-Zarara” (kiza) cha usiku wa manane usiokuwa na mwanga wa kuanzia maisha mapya.

Kazi ni kazi

Wanaomjua toka nyakati zake za ujana wakati alipoteremka Pwani kutoka maeneo yao ya Kibwezi, wanakubaliana nasi kwamba Kalembe ni mchapa kazi na wala hachagui kibarua. Akiwa Mombasa maeneo ya Jomvu miaka ya themanini (1980s) anatambulika na kukumbukwa na wafanyakazi wenzake katika kampuni ya Bayusuf and Sons Transporters na shirika moja lisilo la serikali (NGO) la Makueni kuwa mhudumu mzuri wa kupika chai na mtumishi wa kutumwa hapa na pale (mshenga) ama kwa kimombo –Tea boy-cum-Office Messenger.

Baada ya kuwekwa kwa baridi na serikali ya Jubilee iliyomeza riziki yake (TIP TIP), hali ya maisha na madeni ambayo kila mwanasiasa ni lazima kuwa nayo baada ya uchaguzi, ikamsukuma kuwakera viongozi waliokuwa karibu naye wakati wa kampeini. Wa kwanza ambaye hakupata usingizi katika kipindi chake chote cha ubaridi wa nje ya siasa, ni Gavana wa Nairobi, Mike Sonko ambaye Kalembe Ndile daima alimsukuma aweze kumsaidia aidha kwa kushinikiza Uhuru ampe kazi ama yeye angalie vile anaweza kumsitiri.

Kalembe Ndile katika makao makuu ya cha cha Jubilee baada ya kukivunja chama chake.

Muda wote huu, alikuwa ameshakatiziwa kupiga hodi ikulu ya Rais kama ilivyo kwa wanasiasa wengine wote waliojipendekeza kabla ya uchaguzi mkuu uliopita. Yaaminika kile ambacho amekuwa akinung’unika kila siku, ni majuto ya kufilisi chama chake bila kufaidi kama walivyoagana na wakuu wa Jubilee 2017. Twasikia, kupitia kwa marafiki wake, baada ya kulalamika sana juu ya suala hilo, aliweza kufaulu kupata tu siyo zaidi ya shilingi laki sita (600,000) kutoka kwa matanga ya chama chake cha TIP TIP.

Waliomuona Kalembe chini ya jengo la Anniversary Towers katika uchaguzi mkuu wa 2013, akitumia gari lake aina ya Pick-up kama afisi ya TIP TIP nje ya jengo la Maendeleo ya Wanawake jijini Nairobi akiwauzia wagombea viti waliokosa vyeti kwa vyama vingine vya kisiasa, ama kwa hakika wanamcheka leo kwani siku hizo alitengeneza pesa taslimu zaid ya laki sita alizopewa kwa kuua chama.

Mhudumu wa baa

Maji ya maisha yalipomjaa pomoni na gavana Sonko naye alipochoka kumsitiri mahitaji yake ya maisha kila kukicha, aliamua kumshawishi amhudumie kwenye mkahawa wake anaojivinjari na wageni wake anapokuwa pwani, katika maeneo ya Kikambala, kaunti ya Kilifi. Alijiua hata Rais Uhuru Kenyatta akinusa hizo habari kwamba aliyekuwa kinara wa chama cha TIP TIP na rafiki yao aliyesaidia kumpasha kiongozi wa Wiper wakati wa kampeini za Jubilee na NASA, atamuonea huruma amsunde (kumtafutia) mahala popote serikalini.

Kwa wale hawajui, leo wajue. Kabla ya Rais Uhuru Kenyatta kumteua majuzi kuwa mkurugenzi wa shirika la kusimamia maji la Tanathi – Water Works Development Agency alikuwa ni mhudumu wa baa katika mkahawa wa gavana Mike Sonko katika makao yake ya pwani (eneo la Kikambala, Kilifi).

Kama kawaida yake, wengi waliomkuta hapo aliwakaribisha vyema bila kuona aibu kwa kuwa mwanaume yeyote kazi ni kazi bora kunapatikana riziki. “Je, wajua kuwa mheshimiwa Kalembe Ndile ameajiriwa katika baa la rafiki yake Sonko?, aliuliza mwanasiasa mwenzake ambaye naye alianguka pamoja naye kwenye uchaguzi wa 2017 akiwania ubunge wa Kilifi Kusini.

Safari ya Kalembe Ndile

Kama kawaida ya kijana wa jamii yake ya Wakamba alianzia kazi yao ya ukoo kuziba na kutengeneza matairi ya gari mji wa Kibwezi, katika barabara kuu ya Mombasa-Nairobi. Akiwa barabarani, alikutana na madereva wa kampuni mashuhuri wakati huo ya Mombasa ya Bayusuf & Sons Transporters amabo walimrai aje atafute kibarua pwani.

Alianza kama kijana wa kupikia chai wafanya kazi wa afisini na kutumia wakati wake wa mapumziko kuchonga viti vya maguu matatu akiwa maeneo ya Changamwe. Baadaye akapeleka ujuzi wake wa mtumishi wa afisi (Office Messenger) kwa shirika lisilo la serikali (NGO) akiwa Makueni kati ya mwaka 1984 mpaka 1988.

Kutokana na bidi yake ya maisha na huduma kwa jamii, Kalembe Ndile hakubakia hapo, alijizatiti hadi kuwa diwani akianzia siasa za majuu kwani ni wakati huo ambapo aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa baraza la Wilaya ya Makueni kati ya 1994-1996.

Baadaye, madaraka yalizidi kupanda kwake kwani kati ya 1996-1997 alikuwa mcha Mungu mkubwa hadi akapewa cheo cha mweka hazina katika kanisa la Makueni Catholic Parish Church. Kutoka hapo akachaguliwa kuwa afisa msimamizi wa mipango katika shirika lingine la kijamii la Makueni Paralegal Coordinating Agency.

Hatimaye alijiunga na shirika lingine la Nguluwa Ngao Centre kama msimamizi mkuu ambapo ndipo alianzia kupasha makali ya kujibwaga nayo kisiasa ya kitaifa.

 

Alisimamia shirika hili kuanzia 1997 hadi 2002 wakati alipochaguliwa kuwa mbunge wa Kibwezi hali ambayo wengi wanasema ilichangiwa na ucheshi na ukakamavu wake wa utendaji kazi. Kalembe huwa hajali ni wapi, lini ama vipi kazi itafanywa mradi tu apewe nafasi.

Siasa ya 2002 ambayo iliporomoshwa na NARC dhidi ya KANU ndiyo iliyomtambulisha Kalembe Ndile kwa Wakenya. Machachari yake na mbwembwe za kisiasa ndizo zilizompa umaarufu wakati wa serikali ya NARC.

Uwaziri

Akiwa mbunge wa Kibwezi, Kalembe pia alizawadishwa uwaziri mdogo wa utalii na wanyama pori na vioja vyake vyakumbukwa kwenye majibizano yake na waziri wake wakati huo, Morris Mwachondo Dzoro. Daima Kalembe alikwaruzana na waziri wake kwamba hampangii kazi vyema kama naibu wake na mara kwa mara alisimama kidete kikazi yake.

Alihudumu uwaziri huo hadi kipindi chake kumalizika mnamo 2012 wakati uchaguzi mkuu uliwadia. Wakati alipoona kwamba siasa za vyama hazieleweki na isitoshe Mwai Kibaki anastaafu, aliamua kuanzisha chama chake cha TIP TIP na kuwa mwenyekiti wake wa kitaifa hadi kuzikwa kwa chama hicho na Jubilee mwaka 2017.