Polisi adaiwa kuibiwa bunduki na kahaba

Mshukiwa Jackson Vuti Muthangya akiwa mahakamani baada ya kudaiwa kuiba bunduki na rununu ya afisa wa polisi. Amezuiliwa kwa siku 15 hadi polisi wakamilishe uchunguzi wao dhidi yake. Picha: Kelvin Karan.

Afisa wa polisi ambaye alipoteza bunduki yake anadaiwa kuibiwa bunduki hiyo na kahaba, kisha kumsingizia mhudumu wa bodaboda. Afisa huyo ambaye hakutajwa kwenye nakala za kuomba mahakama kumzuilia mhudumu huyo wa bodaboda anaaminika kuchukua kahaba ambaye alimwibia bunduki pamoja na simu yake ya mkono, kisha kudai kuwa mhudumu huyo alijua kahaba huyo. Maafisa wa polisi walitaka Mahakama kupitia Hakimu Mkuu Edna Nyaloti kumzuilia Jackson Vuti Muthanya kwa siku ishirini ili kukamilisha uchunguzi wa wizi huo dhidi yake.

Kulingana na kiongozi wa mashtaka Eric Masila, mshukiwa alikamatwa baada ya kubainika kuwa alikuwa amepokea shilingi 1, 450 kutoka kwa simu ya Afisa huyo wa polisi na kuwa kuzuiliwa kwake kutasaidia sana katika uchunguzi. Hata hivyo mhudumu huyo wa Bodaboda ameambia mahakama kuwa yeye hausiki na wizi wowote, na kuwa huenda afisa huyo aliibiwa na kahaba. Mhudumu huyo ameambia mahakama kuwa Afisa huyo alipopigiwa simu na wenzake wakati walipokuwa wakimkamata alidai kuwa walikuwa na bibiye katika makao ya polisi na kuwa walilala naye kasha bibiye akamwibia alipokuwa amelala.

Kula uroda

“Polisi walipokuja kunikamata walimpigia polisi mwenzao ambaye anadai kupoteza bunduki na akawa akisema kuwa walilala na bibi yangu katika kambi ya polisi. “Baada ya kufika na kumtazama bibi yangu alidai kuwa siye mwanamke ambaye walikuwa na yeye usiku ambao bunduki yake ilipotea,” Mhudumu huyo wa bodaboda aliambia mahakama.

Alisema kuwa yeye alibeba abiria kama kawaida ambaye alidai kuwa hakuwa na hela mfukoni na kutaka mahali ambapo angeweza kutoa pesa kupitia M-Pesa na abiria huyo akamtumia pesa ili atoa na kumkabidhi malipo yake, akisema kuwa hawezi kuwakumbuka abiria wote ambao huwa anawabeba. Hakimu Mkuu Bi. Nyaloti alikataa ombila upande wa Mashtaka kutaka maafisa wa polisi kumzuilia mhudumu huyo kwa siku Ishirini. “Mshukiwa atazuiliwa kwa siku kumi na tano ili maafisa wa polisi wakamilishe uchunguzi wao na mshukiwa atarudishwa tena hapa mahakamani tarehe 27 mwezi huu,” asema Bi. Nyaloti akitoa uamuzi wa Mahakama.