Ni mwelekeo upi Rais Uhuru anao ndani ya 2022?

Kama njia mojawapo ya kuzima uhasama wa umiliki wa eneo lake la kati, Rais Uhuru Kenyatta aliwaalika kwenye mkutano wa faragha zaidi ya viongozi 3000 kwenye Ikulu ya Sagana.

Kenyatta pia alitumia nafasi hiyo kusisitiza kwamba ushirikiano wake na Raila Odinga chini ya BBI ni wa kuhakikisha kwamba hakutatokea tena ghasia za baada ya uchaguzi mkuu siku za usoni.

Rais anasema kwamba walipokubali kuamkuana na Raila hakumpa ahadi angemuunga mkono wakati atakapotaka kugombea Urais na wala swala la siasa za 2022 halikuwapo kwenye makubaliano wakati wa mazungumzo yao maarufu “handisheki”.

Hata hivyo Rais aliwashangaza wengi wanaotumaini kwamba atang’atuka uongozini baada ya uchaguzi mkuu ujao wa maka 2022 kwa kutangaza kwamba amekubali maoni ya wengi hasa wandani wake wa kisiasa wanaopendekeza marekebisho ya kikatiba kufanyika kubuni nafasi au cheo cha waziri mkuu ili kumpa nafasi kuongoza kwa muhula mwingine.

Rais aliyeonekana kushangazwa na malumbano baina ya viongozi kuhusu ripoti ya BBI inayotarajiwa kutolewa kwa umma hivi karibu. Aliwataka viongozikwanza kumuunga mkono kwenye uongozi wake kwani anafahamu kinachowafaa.

“Sina ufahamu wa kile kilicho kwenye ripoti ya jopokazi la maridhiano BBI bali naskia watu wakisema Uhuru anataka kuwa waziri mkuu. Sitojali kuhudumu uongozini kwenye wadhifa huo, lakini tujishughulishe kwanza na maswala ya sasa,” alisema Rais Kenyatta.

Katiba ya mwaka 2010 haishirikishi mfumo wa bunge ama serikali inayoongozwa na waziri mkuu ingawaje duru zinaarifu kuwa mapendekezo yaliyokusanywa na tume ya BBI yanajumuisha yale ya kuwepo mabadiliko ya katiba kupitia kura ya maamuzi kubuni nafasi ya waziri mkuu.

Aidha mawaziri watateuliwa kutoka kwa wabunge waliochaguliwa tofauti na ilivyo sasa ambapo wabunge ni wawakilishi na watunzi wa sheria ilihali mawaziri wanachaguliwa nje ya bunge kuongoza wizara za serikali.

Rais aidha alichagua kuwanyamazisha wana “Tanga Tanga” kutoka eneo la kati wanaoeneza dhana kwamba Kenyatta amemuasi naibu wake William Ruto kwa kusema kutotangaza kumuunga mkono mwaka 2022 na badala yake anapanga kubuni muungano na Raila Odinga.

Hatua ya Rais ya kuchukua usukani wa kuzunguka na wakuu wengine kwenye uongozi wa taifa kupigia debe mapendekezo ya ripoti ya BBI inaonyesha bayana kwamba anaunga mkono kwa kina yaliyo kwenye ripoti hiyo, ingawaje rais amesema mara si haba kwamba yeye binafsi anamchango wake maalum atakaoutoa kama njia ya kujitolea kwake kufanikisha kujenga Kenya yenye nafasi huru kwa wote.

Viongozi wa eneo la kati mwa nchi walitumia fursa hiyo ya kukutana na Rais Kenyatta kuwasilisha orodha ya matakwa ya watu wa eneo la mlima Kenya wakati ambapo baadhi yao walilalamikia hatua ya rais kuipa kipaumbele maendeleoya katika maeneo ambayo hayakumuunga mkono mwaka wa 2017 kwenye uchaguzi wa urais.

Naibu wa rais William Ruto ameonekana kupendezwa na hatua ya rais ya kufanya mkutano wa faragha na viongozi wa eneo la kati huku akiyaunga mkono matamshi ya Rais akiongeza kwamba viongozi walio na nia ya kukigura chama cha jubilee waondoke chamani badala ya kusalia vugu vugu. “Wanatakikana waamue wanakotaka kuwa.

Haiwezekani kuwa kila mahali. Wapange hatima yao ya kisiasa badala ya kukubali kutumiwa kuleta mgawanyiko katika chama cha Jubilee,” alisema Ruto.

Wakenya mbali mbali kwenye mitandao ya kijamii wametoa maoni toauti tofauti kuhusu mkutano wa Viongozi wa eneo la kati na kauli ya Rais kuhusu wadhifa wa waziri mkuu baada ya mhula wake wa pili kukamilika mwaka wa 2022, ingawaje wengi wameipokea hatua hiyo kama njia ya kukabili upinzani ndani ya jubilee.

Wapo wanaoshikilia kwamba Rais ni kiongozi wa taifa na hana shinikizo lolote dhidi yake kukutana na kabila moja pekee badala yake viongozi wa kati wangebuni njia mwafaka ya kuyashughulikia matakwa yao pasipo na kumvuta rais hadi kiwango cha eneo.

Wandani wa Uhuru Kenyatta na hasa kutoka kabila lake wanadai kwamba bado umri wake ni mdogo mno kuondoka uongozini na hivyo atafutiwe nafasi ya kuendelea kuongoza wakenya na hiyo si nyingine bali ile ya waziri mkuu ambayo inaweza kubuniwa tu kupitia mabadiliko ya katiba.

Ikiwa azma hiyo itatimia Uhuru Kenyatta atakuwa waziri mkuu wa tatu baada ya baba yake Mzee Jomo Kenyatta kushikilia wadhifa huo kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mwaka 1963 hadi 1964 ambapo wadhifa huo ulifutiliwa mbali na baadaye kurejeshwa wakati wa mkataba wa ugavi wa mamlaka uliotiwa baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 uliozua ghasia naye kiongiozi wa upinzani Raila akashikilia wadhifa wa Waziri Mkuu.

Mdahalo wa kubuniwa kwa wadhifa wa Waziri Mkuu umeonekana kushika kasi huku wadadisi wa maswala ya kisiasa wakiitaja hatua hiyo kama ulafi wa viongozi wa barani Afrika ambao tamaa yao ni kusalia mamlakani hata baada ya vipindi vyao vya uongozi kukamilika.