Mwanahabari Jacque Maribe na mpenziwe, Joseph Kuria lrungu maarufu Jowie, wakanusha mashtaka ya mauaji ya mfanyabaishara, Monica Kimani

Mwanahabari Jacque Maribe na mpenziwe, Joseph Kuria lrungu maarufu Jowie, wamesomewa upya mashtaka ya mauaji ya mfanyabaishara, Monica Kimani ambapo wamekana mashtaka dhidi yao.

Wawili hao wamekana kuhusika mauaji hayo mnamo Septemba 19 mwaka uliopita katika nyumba za Lamuria Gardens Mtaani Kilimani, jijini Nairobi , wakati Monica aliporejea nchini kutoka Sudan Kusini alikokuwa akijihusisha na biashara ya familia.

Katika mashtaka hayo mapya, upande wa mashtaka ulibadili stakabadhi za mahakama na kulijumuisha jingine la utani la Jowie ambalo ni Harun. 

Upande huo vilevile uliwasilisha taarifa kuhusu masuali unayotaka yajibiwe kuhusu mauaji ya Monica.

Hata hivyo kisanga kilishuhudiwa wakati mawakili wa upande wa utetezi walipopinga uamuzi wa upande wa mashtaka kuionesha mahakama baadhi ya picha za Monica,  ukisema hatua hiyo ilikuwa ya kupoteza muda wa mahakama ambapo upande wa mashtaka ulijitetea kwa kusema kwamba, hatua ya kuonesha picha hizo ni kudhihirisha  kwamba ofisi ya Mkuu wa Mashtaka ya Umma, DPP inakumbatia teknolojia katika utendakazi wake.

Kufikia leo saa nane  adhuhuri, upande wa mashtaka ulikuwa umewasilisha mashahidi wawili, mmoja akiwa daktari aliyeufanyia uapsuaji mwili wa Monica na kubainisha alifariki dunia kwa kutokwa na damu nyingi kufuatia jeraha shingoni, huku shahidi wa pili akiwa afisa wa polisi aliyewasilisha picha za eneo la tukio. Jumla ya mashahidi 32 wananuiwa kuwasilisha ushahidi wao.