Maafisa zaidi watumwa North Rift kuimarisha usalama

Oparesheni kali ya Usalama inatarajiwa kuanza eneo la North Rift baada ya maafisa wa polisi kutumwa eneo hilo. Waziri wa Usalama na Masuala ya Ndani ya Nchi Fred Matiangi amewatuma maafisa hao wakiongozwa na Mkuu wa Kitengo cha Maafisa wa Kukabili Ghasia GSU kiongoza oparesheni kwenye kaunti za Baringo, Pokot Magharibi, Samburu, Elgeyo Marakwet, Turkana na Laikipia.

Haya yanajiri kufuatia uvamizi baina ya jamii kwenye kaunti hizo  ambao umesababisha watu kadhaa kuuliwa na mali kuharibiwa. Kadhalika watu kadhaa wamehama makazi hayo. Hapo jana Gavana wa Pokot Magharibi John  Lonyangapuo alikutana na mwenzake wa Elgeyo Marakwet, Alex Tolgos walikutana ili kujadili jinsi ya kurejesha manai huku Lonyangapuo akiwalaumu maafisa wa polisi kwa kukwepa maeneo yenye mizozo hasa msitu wa Embobut.

Haya yanajiri huku taharuki ikiwa imeendelea kutanda katika eneo la KBC, Mjini Marsabit baada ya watu wawili kuuliwa. Kamanda wa Polisi wa Kaunti hiyo Steve Oloo amesema kuwa wawili hao walikuwa wamelala wakati walipovamiwa na watu wasiojulikana waliowapiga risasi vichwani na kuwauwa papo hapo. Oloo amesema washukiwa wa mauaji hayo wangali wanatafutwa na watakapopatikana wachukuliwa hatua za kisheria.

Ikumbukwe Jumatatu wiki hii shule nne zilifungwa enei la Arabal  Baringo Kusini baada ya wavamizi waliojihami kuivamia nyumba moja na kuwajerihi watu wawili kisha kutoweka na mifugo mia moja.

Kwenye Kaunti ya Laikipia viongozi wameilaumu serikali kwa kuwapokonya silaha maafisa wa akiba KPR hali ambayo imesababisha kuongezeka kwa utovu wa usalama. Wabunge hao wametishia kujichukulia sheria mikononi kuwakabili washukiwa wa wizi wa mifugo iwapo serikali haitadumisha usalama.