IEBC yaansa kumtafuta Afisa Mkuu Mtendaji mpya

Tume ya Uchaguzi, IEBC imetangaza nafasi ya Afisa Mkuu Mtendaji kuwa wazi huku ikiwashauri Wakenya kutuma barua za maombi ya kazi. Tangazo hilo linawashauri Wakenya kutuma maombi kati ya leo na tarehe tatu mwezi ujao.

Nafasi hiyo iliachwa wazi baada ya aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji katika tume hiyo, Ezra Chiloba kufutwa kazi baada ya kusimamishwa kazi kuanzia mwezi Aprili mwaka jana.

Chiloba alifutwa kazi rasmi tarehe 24 mwezi Septemba mwaka uliopita baada ya ripoti ya IEBC kuashiria kwamba alitumia mamlaka yake vibaya hali iliyosababisha kupotea kwa mamilioni ya fedha wakati wa uagizaji wa vifaa vya kupigia kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2017.

Kwasasa IEBC ina makamishna watatu ambao ni Mwenyekiti Wafula Chebukati, na makamishna Boya Molu na Abdi Guliye. Aidha makamishna Roselyn Akombe, Connie Maina, Paul Kurgat na Margaret Mwachanya walijiuzulu wakikakamikia uongozi wa Chiloba wakiutaja kuwa wa kiimla.