Mjadala mkali umeibuka baada ya Naftali Kinuthia kukana kumua Ivy Wangeci

 

Baada ya mshukiwa mkuu wa mauaji ya Ivy Wangeci - mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Moi Eldoret, Naftali Kinuthia kukana mashtaka, mjadala mkali uliibuka katika mitandao ya kijamii. Wengi wanasema kuna walioshuhudia kisa hicho na Naftali mwenyewe alikiri mbele ya Mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Eldoret Ali Kingi kumuua Ivy, iweje anakana sasa mbele ya jaji?

Kabla mshukiwa kufika mahakamani anastahili kushauriana na wakili wake iwapo atakiri makosa au la kwa vile ukikana mashtaka inaaminika hukumbuki kilichotokea, unatarajia upande wa mashtaka kutoa ushahidi utakaokuhukumu au ni kweli huna makosa.


Vilevile, kabla ya kukana mashtaka unastahili kujua uzito wa kesi hiyo, kinachostahili kuthibitishwa na maafisa wa polisi na hukumu iwapo utapatikana na kosa hilo.

Anavyoeleza wakili Mark Oloo mtu akishtakiwa kwa kosa la mauaji anaweza kukana mashtaka iwapo tukio hilo lilitokea bila kukusudia na hakuwa na nia ya kuua.

Hata hivyo katika kisa cha Naftali, wengi wanadai kuwa kuna uwezekano mkubwa alikuwa na nia ya mauaji kwani alisafiri kutoka Nairobi hadi Eldoret kwenye kumuua Ivy.

Hata hivyo kwa baadhi ya kesi, na kulingana na uzito wa kesi wakili anaweza kumshauri mshukiwa akiri mashtaka.
 

Hata hivyo mshukiwa anapokana kesi hiyo uahirishwa kwa muda ili upande wa mashtaka utayarishe ushahidi. Wakati kesi itakapoendelea, hakimu atasikiliza ushahidi wote kabla ya kutoa hukumu. Iwapo baada ya kukana mashtaka mshukiwa anataka kukubali anastahili kufanya hivyo kabala tarehe ya kesi hiyo ili kuwazuia mashahidi kufika mahakani na kutolipishwa ada.

Hata hivyo, upande wa mashtaka unaweza kuwa makubaliano na mshukiwa kumpunguzia hukumu.
 

Katika kitengo 137 A-O, za sharia za uhalifu nchini, mashukiwa anaweza kupunguziwa hukumu anapokubali mashtaka pekee. Katika kitengo cha 137 E, makubaliano hayo hufanyika mshukiwa anapokubali kuwa shahidi wa upande wa serikali, mshukiwa anapokubali kumfidia aliyewasilisha mashtaka, kunapokuwa na makubaliano ya kupunguziwa kifungo, miongoni mwa makubaliano mingine.

Hata hivyo kwa mujibu wa kitengo 137K mshukiwa anaweza kukana makubaliono iwapo hakuelewa mkataba, ahadi alizopewa hazikuafikiwa, hakuwa katika hali sawa kiakili au alilazimishwa, lakini mabadiliko hayo yanastahili kufanyika kabla yafike mahakani au baada ya kurekodi kukukiri mashtaka lakini hukumu bado haijatolewa na hakimu.
Vilevile kwa mujibu wa kitengo 137M, makubaliano hayo hayawezi kutumiwa dhidi ya mshukiwa wakati wowote ila yanastahili kupunguza kiwango cha hukumu pekee.

Hata hivyo, makubalino hayo si ya kesi zote, kesi za ubakaji, mauaji ya halaiki, na uhalifu unaokiuka haki za binadamu huwa hazina makubaliano.

Changamoto kuu ya makubalino hayo huwa, katika baadhi ya kesi mshukiwa ambaye hakufanya kosa hulazimishwa kukubali ili kupunguziwa kifungo, mshukiwa analazimika kutoa ushaidi wa uongo ili apunguziwe kifungo, wengi huamini makubalino hukiuka haki ya mshukiwa kuwa hauna makosa hadi upande wa mashtaka uthibitishe na katika baadhi ya kesi mawakili wanalazimika kumshawishi mshukiwa kukubali kufuatia matakwa ya mteja aliyewasilisha kesi jambo ambalo huwaweka mawakili wengi katika njiapanda.

Baada ya kukana mashtaka, kesi dhidi ya Naftali Kinuthia imeahirishwa hadi tarehe 10 mwezi Juni ili kuipa upande wa mashtaka muda wa kukusanya ushahidi.